HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma imepangiwa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula(NFRA) katika msimu huu kununua mahindi tani 400.Afisa Kilimo wa Manispaa ya Songea Mushoborozi Christian amesema Halmashauri hiyo imepokea barua toka NFRA inayotoa maelekezo ya ununuzi wa mahindi katika awamu ya tatu msimu wa mwaka 2017/2018.
Amesema katika Manispaa ya Songea Kata saba tu kati ya Kata 21 zinaruhusiwa kununua mahindi katika kituo cha NFRA ambapo wananchi wanatakiwa kupeleka mahindi kwa ajili ya kuuza.Mushoborozi anazitaja Kata ambazo zinahusika katika ununuzi wa mazao hayo kuwa ni Lilambo ambayo imepangiwa kununua tani 100,Subira 100,Mjimwema 40,Ruhuwiko 60,Mshangano 40, Matogoro 30 na Ndilimalitembo tani 30 hivyo kufanya jumla ya tani 400.
Hata hivyo Mtaalam huyo wa kilimo amewaasa wananchi wote wanauza mazao hayo,kuhakikisha mahindi wanayopeleka kuuza yasiwe na uchafu ili kuondoa usumbufu na kwamba wananchi wanatakiwa kuuza mahindi kulingana na mgawo wa ununuzi kwa kila Kata husika.“Kumekuwepo na tabia ya baadhi ya Kata kutofikia malengo ya serikali ya kuuza mahindi NFRA,katika awamu hii Afisa Mtendaji wa Kata atakayeshindwa kuhamasisha wakulima kuuza mahindi NFRA atawajibishwa’’,anasisitiza Afisa Kilimo huyo.
Kulingana na Mtaalamu huyo,Mkulima anaruhusiwa kuuza tani moja tu ya mahindi NFRA na kwamba bei ya kilo moja ni shilingi 500 na kwamba zoezi la kupeleka mahindi NFRA linatakiwa kukamilika Novemba 17.
Imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa