NAIBU Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Josephat Kandege amekagua mradi wa kituo cha Afya kata ya Ruvuma katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea.
Kandege ameagiza ramani ya kituo hicho kufanyiwa marekebisho kwa kutumia ramani mpya iliyotolewa na TAMISEMI na kwamba kwa kuwa mradi upo katika hatua za awali ni rahisi kufanya marekebisho hayo.
Amesema katika ramani mpya Halmashauri inaweza kupanga bei kwa kila hatua na kwamba kwa ramani hiyo unaweza kubadilisha fundi na kuendelea na fundi mwingine iwapo mmeshindana.
Naibu Waziri huyo pia ameagiza kuhakikisha eneo la kituo cha afya lisipungue hekari nane na kuhakikisha kuwa eneo la kituo cha afya Ruvuma lipimwe na kuwa na hatimiliki yake.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Tina Sekambo akitoa taarifa ya mradi huo ambao unaanzia Agosti Mosi hadi Novemba 30,2018,amesema Manispaa imepokea kiasi cha shilingi milioni 400 kutoka serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha Afya kata ya Ruvuma.
Amelitaja lengo la kujenga kituo hicho cha Afya katika kata ya Ruvuma kuwa ni kuboresha huduma bora za afya kwa wananchi wa kata hiyo wapatao 17,536.
Hata hivyo amesema kituo hicho kikikamilika kinatarajia kutoa huduma kwa wananchi 45,923 waliopo katika kata nne za Subira,Mateka,Majengo na Ruvuma.
“Kituo hiki kintarajia kupunguza maradhi sugu yanayowasumbua wananchi wa kata ya Ruvuma yakiwemo malaria,kuhara,kifua kikuu,UKIMWI na magonjwa ya njia ya mkojo na vichomi’’,anasisitiza Sekambo.
Kwa mujibu wa Sekambo,kituo hicho kinatarajiwa kuwa na majengo ya wodi ya akinamama,jengo la upasuaji, maabara,jengo la mapokezi,kuchomea taka,shimo la kutupia kondo la nyuma na shimo la kuhifadhia majitaka.
Katika kuhakikisha kazi inafanyika kwa ufanisi mkubwa,Sekambo amesema,Halmashauri imefanya uteuzi wa kamati tatu ambazo ni manunuzi,mapokezi na ujenzi kulingana na mwongozo wa TAMISEMI na kwamba kamati zimeundwa kwa kushirikisha jamii husika na wataalam wa Halmashauri.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Alhaji Abdul Hassan Mshaweji amemshukuru Rais Dkt.John Magufuli kwa kuipatia Manispaa hiyo fedha za ujenzi wa kituo cha afya kata ya Ruvuma.
Imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari wa Manispaa ya Songea
Simu 0784765917
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa