Na AMINA PILLY
AFISA HABARI – MANISPAA YA SONGEA
Halmashauri ya Manispaa ya Songea imeweka mkakati wa utekelezaji wa Sera, Programu ya kilimo cha Kibiashara na Manufaa kwa Wananchi ambapo ili kufanikiwa utekelezaji wa mkakati huo Manispaa ya Songea imeweka utaratibu wa uanzishwaji wa kilimo cha Pamoja (Block Farming) kwa wakulima wa Manispaa ya Songea, chenye ukubwa wa mashamba kuanzia ekari 500 na zaidi.
Utekelezaji wa Mkakati huo umetokana na agizo la Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge ambaye ameelekeza Halmashauri zote Mkoani Ruvuma kuandaa na kuanzisha kilimo cha Mashamba Makubwa kuanzia ekari 500 na Zaidi (Block Farming), ambapo kutokana na Master Plan ya Manispaa ya Songea, Maeneo yaliyo ainishwa kwa shughuli za kilimo hicho yanapatikana katika kata nne (4) ambazo ni Tanga, Lilambo, Mletele na Subira.
Block Farming ni mfumo/utaratibu wa kulima kwa pamoja kwa kuunganishwa mashamba na kuwa katika block moja ambapo wakulima wanapatiwa huduma za kilimo ikiwemo pembejeo, huduma za ugani, zana za kilimo, na kupewa mafunzo kwa pamoja.
Kwa mujibu wa maelekezo hayo, mashamba Makubwa (Block Farming) ya pamoja yatawawezesha wakulima kupata huduma za ugani, matumizi ya zana bora za kilimo pamoja na misaada mingine ikiwemo miundombinu wakiwa katika eneo moja kubwa.
Amewataka wananchi wote wa Manispaa wenye maeneo makubwa kuanzia hekari 500 na zaidi, wajitokeze kwa wingi ili kushiriki kilimo cha pamoja kwa mazao ya Soya na alizeti ambazo zitasaidia kukuza uchumi kijamii na Taifa kwa ujumla.
Endapo Mkulima hatakuwa na uwezo wa kulima Hekari zote moja kwa moja anashauriwa kushilikiana na wakulima wengine wenye mashamba ili kutafuta wawekezaji, au taasisi mbalimbali zikaja kulima katika maeneo hayo kwa makubaliano maalumu na utaratibu mzuri ambao utaleta mafanikio.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa