Halmashauri ya Manispaa ya Songea imeendesha semina elekezi kwa Waheshimiwa Madiwani Manispaa ya Songea yenye lengo la kuwajengea uelewa juu ya masuala mbalimbali ya uongozi ikiwemo na namna ambavyo serikali za mitaa zinaendeshwa na majukumu yake.
Kwa mujibu wa katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika Ibara ya 145(1) inasema “Kutakuwa na vyombo vya Serikali za Mitaa katika kila Mkoa, Wilaya, Mji, na Kijiji” kwa lengo la kupeleka madaraka na huduma kwa Wananchi ili kuleta maendeleo katika jamii husika.
Semina hiyo imetolewa leo tarehe 07.05.2021 katika ukumbi wa Manispaa ya Songea na kuhudhuliwa na Waheshimiwa Madiwani wa kata zote 21 zilizopo Songea Mjini ambapo wamefundishwa taratibu za hatua za kinidhamu kwa watumishi wa mamlaka za serikali za mitaa, taratibu za mikutano na uendeshaji wa shughuli za Halmashauri, Majukumu ya Mstahiki Meya, Madiwani na Wenyeviti wa Mitaa, pamoja na Mfumo wa fursa na vikwazo kwa maendeleo (O&OD) ulioboreshwa.
Akiwasilisha mada ya uendeshaji wa Serikali za Mitaa na majukumu yake Wakili wa Serikali ofisi ya Mkuu wa Mkoa Ruvuma Seligius Ngahi amesema kwamba majukumu ya Serikali za Mitaa (Halmashauri) yanajulikana kikatiba ambapo katika Ibara ya 146(1) Katiba inasema “Madhumuni ya kuwapo Serikali za Mitaa ni kuwashirikisha wananchi katika shughuli za maendeleo, kusimamia utekelezaji wa sheria na ulinzi wa wananchi pamoja na kuimarisha demokrasia katika ngazi zake zote” Alibainisha.
Ngahi ametoa wito kwa Waheshimiwa Madiwani wa Manispaa ya Songea kutumia fursa itakayowajengea uelewa zaidi juu ya kutekeleza majukumu yao kama sehemu ya wawakilishi wa wananchi kwa Serikali kuu ili kupeleka maendeleo katika maeneo yao. ‘Ngahi alisisitiza’.
Naye Afisa Utumishi ofisi ya Mkuu wa Mkoa Ruvuma Zuberi Msham ametoa muongozo wa posho na stahiki za Waheshimiwa Madiwani ikiwemo na posho za usafiri, kujikimu, posho ya madaraka na ya mwezi.
Kwa upande wao Waheshimiwa Madiwani wa Manispaa ya Songea wameishukuru Halamshauri ya Manispaa ya Songea kwa kuandaa mafunzo haya kwa sababu yamewasaidia kujua majukumu yao ya msingi, utawala bora, uwajibikaji, na kutambua stahiki zao.
Pia wametoa ombi kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea kuendelea kutoa mafunzo mara kwa mara ili kuwajengea uelewa juu ya masuala ya utawala bora, nidhamu, namna ya kushirikisha wananchi katika uibuaji wa miradi ya maendeleo katika jamii.
Mpaka sasa Halmashauri ya Manispaa ya Songea imekuwa ni Halmashauri pekee iliyotoa mafunzo kwa Waheshimiwa Madiwani kati ya Halmashauri nane Mkoani Ruvuma.
IMEANDALIWA NA,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA,
07.05.2021.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa