MWENYEKITI wa Bodi ya Shirika la Miracle Corner Tanzania (MCT) Halima Mamuya na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Alhaj Abdul Hassan Mshaweji wamesaini mkataba wa kukabidhi ardhi yenye ukubwa wa ekari 50 katika eneo la Kipera kata ya Ruvuma ikiwa na thamani ya shilingi bilioni 1.2.Mkataba wa makabidhiano hayo umefanyika katika Ofisi ya Mstahiki Meya Mjini Songea.
Akizungumza mara baada ya kusaini mkataba huo,Mwenyekiti huyo wa Bodi ya MCT amesema walikabidhiwa ardhi hiyo na Manispaa ya Songea mwaka 2004 ikiwa haina kitu ambapo hivi sasa wanairudisha tena ardhi hiyo katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea wakiwa wameliendeleza ili kuiendeleza na kufanya mambo makubwa zaidi na kwamba MCT ipo tayari kuendelea kushirikiana na serikali katika sekta za afya na elimu.
Programu hii ya dental hatutaiacha tutaendelea nayo,tunatarajia eneo hili litakapojengwa kuwa hospitali,tupo tayari kushirikiana na Manispaa ya Songea kuliendeleza kwa manufaa ya wananchi wa manispaa ya Songea na mkoa wa Ruvuma kwa ujumla'',amesisitiza Mamuya.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Alhaj Abdul Hassan Mshaweji amelipongeza shirika la MCT kwa kuikabidhi ardhi hiyo Manispaa ya Songea ikiwa thamani yake imepanda na kusisitiza kuwa manispaa ya Songea hivi sasa ipo katika mkakati wa ujenzi wa zahanati kila mtaa na Kituo cha afya kila kata hivyo eneo hilo wanatarajia kulitumia kujenga hospitali ya wilaya ambayo haipo katika Manispaa ya Songea.
Mshaweji amesema MCT kutoa kipaumbele katika eneo la afya ya meno ,kumechangia kwa kiwango kikubwa kwa sababu watanzania wengi hawajatoa mwamko mkubwa katika afya ya meno na kinywa ambayo ni muhimu katika ustawi wa jamii ya watanzania na kwamba Baraza la Madiwani limepokea eneo hilo kwa mikono yote miwili na kwamba MCT imetoa mchango mkubwa kwa serikali na kutoa rai kushirikiana na Manispaa wakati wa kuliendeleza eneo hilo.
Naye Jane Shuma ambaye ni Meneja wa MCT akizungumzia historia ya eneo anasema shirika hilo lilijenga kliniki ya meno ambayo inaendelea kutumika,pia shirika limejenga kituo cha kuhudumia jamii na nyumba 12 zimejengwa kwa ajili ya wafanyakazi na vijana na kwamba eneo hilo katika kipindi chote limekuwa muhimu kwa maendeleo ya vijana na kwamba wakati wanakabidhiwa eneo hilo lilikuwa tupu na halijaendelezwa ambapo hivi sasa wanalikabidhi katika manispaa ya Songea eneo hilo llikiwa limeendelezwa na kwamba anamatumaini makubwa kuwa eneo hilo litaendelea kutoa huduma za afya na elimu.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Oktoba 24,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa