Na,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
08.12.2021
Halmashauri ya Manispaa ya Songea yajipanga kuanza ujenzi wa soko la kisasa Manzese A ifikapo Julai 2022.
Hayo yamebainishwa na Mratibu Msaidizi wa Kitengo cha Uratibu wa Miradi ya Benki ya Dunia cha Ofisi ya Rais - TAMISEMI (WBCU) Rashid Mtamila wakati akitoa mafunzo kuhusiana na utekelezaji wa mradi wa kuboresha miundombinu na utendaji kazi ndani ya Halmashauri za miji (TACTIC), kwa wataalamu na viongozi mbalimbali wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea leo tarehe 08 Disemba 2021 katika ukumbi wa Manispaa ya Songea.
Mtamila alieleza kuwa lengo la mradi huo ni kuziboresha Halmashauri ili ziweze kutoa huduma bora kwa wananchi kwa kuboresha miundombinu ndani ya Halmashauri za miji nchini Tanzania ambapo kiasi cha shilingi Trilioni moja na bilioni 150 kimetolewa kutoka benki kuu ya dunia ambazo zitagawanywa katika Halmashauri za miji 45 nchini.
Aliongeza kuwa mgawanyo wa fedha hizo utakuwa katika awamu tatu ambapo awamu ya kwanza fedha hizo zitatolewa kwa Halmashauri za miji 12 ikiwemo na Halmashauri ya Manispaa ya Songea kwa lengo la kuboresha miundombinu ya barabara kwa kiwango cha lami, madaraja, maeneo ya kutupa taka pamoja na ukarabati wa masoko ikiwemo na soko la Manzese.
Akibanisha Halmashauri za miji zitakazonufaika mradi huo kwa awamu ya kwanza ni pamoja na Ilemela MC, Mwanza CC, Geita TC, Kahama MC, Tabora MC, Kigoma ujiji MC, Arusha CC, Dodoma CC,Morogoro MC, Sumbawanga MC, Mbeya CC, na Songea MC.
Alisema kuwa mradi wa TACTIC umelenga kupunguza changamoto ya upungufu wa miundombinu bora katika miji hali inayotokana na ongezeko la watu katika maeneo ya mjini na hivyo kusababisha miundombinu iliyopo kushindwa kukidhi mahitaji ya idadi ya watu inayoongezeka kila mwaka.’Mtamila Alibainisha’
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Sustainability Associate Ltd Kayonko Juma Kayonko amewataka wataalamu wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea kuhakikisha wanawashirikisha wadau mbalimbali ikiwemo na wafanyabiashara pamoja na wakazi wa maeneo hayo kwa lengo la kupata maoni yao kabla ya utekelezaji wa mradi kuanza ili kuondoa migogoro na malalamiko yanayoweza kujitokeza.
Aidha, Mkuu wa kituo kikuu cha polisi Songea SP. Saana Mdatu amewataka wataalamu kuhakikisha wanazungumza na wadau waliopo katika maeneo ambayo miradi hiyo itatekelezwa ili kuweka makubaliano ambayo hayatasababisha uvunjifu wa Amani katika kipindi cha utekelezwaji wa mradi huo.’Alisisitiza’
Akitoa shukrani kwa niaba ya viongozi na wananchi wa kata ya Misufini, Diwani wa kata hiyo Mh. Ismail Azizi ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha hizo kwa ajili ya kuboresha soko la Manzese pamoja na kutengeneza lami kilomita 3 kuzunguka soko hilo ambalo lipo katika eneo la kata yake na kusaidia kuinua uchumi kwa kutoa ajira kwa wananchi waliopo katika eneo hilo.
Naye Katibu wa wamachinga Manispaa ya Songea Mohammed Sulemani alisema kuwa mradi huu utaleta tija kwa wananchi hususani kwa wajasiriamali ambao wataweza kufanya biashara kwenye maeneo mazuri yalioboreshwa.
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa