Na;
AMINA PILLY;
AFISA HABARI MANISPAA YA SONGEA
16 DISEMBA 2021
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Serikali za Mitaa sehemu ya utoaji huduma na Utawala Bora (TAMISEMI) Angelista Kihaga amewataka viongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea kuweka utaratibu wa kufanya vikao mara kwa mara kwa kushirikisha kamati za shule, waheshimiwa Madiwani, Walimu na uongozi wa Serikali za mitaa ili kupokea changamoto zinazoikabili shule hususani miundombinu ya shule.
Hayo yamebainishwa leo tarehe 16 disemba 2021 katika ziara ya siku moja iliyofanyika Manispaa ya Songea yenye lengo la kukagua ujenzi wa madarasa uliokuwa ukisimamiwa na kamati ya ujenzi wa miradi hiyo ili kutekeleza Mpango wa maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya UVIKO 19, ambapo alifanikiwa kutembelea Shule ya Sekondari Matogoro, shule ya Sekondari Msamala, shule ya Sekondari Londoni, shule ya sekondari Lizaboni na Shule ya sekondari Mfaranyaki.
Kihaga amewapongeza viongozi na Wataalamu wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea kwa jitihada za usimamizi bora wa ujenzi wa madarasa 29 yenye thamani ya Shilingi 660,000,000 ambao ulianza tarehe 01 novemba 2021 na kukabidhiwa kwa Mkuu wa Wilaya tarehe 11 disemba 2021 ukiwa tayari umekamilika kwa asilimia 100%. “Kihaga aliwapongeza”
Amewarai Wananchi wote kuendelea kujitolea pamoja na kuchangia nguvu kazi kupitia mitaa yao ili kusaidia kupunguza kero za miundombinu mbalimbali za shule pamoja na kuimarisha hali ya ufaulu wa wanafunzi katika halmashauri.
Amewataka wataalamu wa ujenzi kuendelea kusimamia miradi ya ujenzi yote inayoendelea kujengwa bila kujali upungufu wa wataalamu hao wa ujenzi kwani kwa kufanya hivyo kutakuwa na mafanikio chanya ya utekelezaji kwa kila mradi utakaopangwa kujengwa.
Waheshimiwa madiwani kwa nyakati tofauti nao wametoa shukrani kwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fedha katika Halmshauri na kufanikiwa kujenga madarasa 26 ya Sekondari na madarasa 3 shule za msingi ili kupunguza changamoto za madarasa na samani za shule.
Wanafunzi wa Sekondari na Msingi nao wameipongeza Serikali kwa kuwezesha kujenga miundombinu ya madarasa ambapo walizitaja faida za kuwepo kwa miundombinu rafiki ya kujisomea ikiwemo na uwepo wa ufaulu mzuri, kupata usikivu darasani, pamoja na kuondoa kero ya mlundikano wa wanafunzi wawapo madarasani.
Mwisho
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa