Halmashauri ya Manispaa ya Songea imewainua wakulima wa zao la biashara la Ufuta kwa kuwapatia mbegu bora za ufuta kwa wanavikundi 3 vitatu pamoja na AMCOS ili kuepukana na kutegemea zao moja la mahindi ambalo ni zao kuu la chakula.
Hayo yamebainishwa na Afisa kilimo wa Manispaa ya Songea Zawadi Nguaro katika mafunzo kwa wanavikundi vya wakulima wa ufuta kutoka kata ya Lilambo,Mletele, Subira, pamoja na kikundi cha wakulima wa AMCOS Songea yanayoendeshwa na Halmashauri ya Manispaa ya Songea, ambayo yanayoendelea kufanyika kwa muda wa siku tatu kuanzia 23 – 25/11/2020.
Nguaro “ alisema Halmashauri ya manispaa ya Songea ina kata 21, kati ya kata hizo ni kata tatu ambazo zimeanza kupata mafunzo kwa wanavikundi wa kilimo bora cha ufuta kwa lengo la kutoa elimu kwa wakulima ili waweze kulima zao bora la biashara la ufuta kwa ajili ya kuinua kipato cha mkulima na kuondoa dhana ya kulima zao moja la mahindi pekee.
Alisema kazi ya Halmashauri ni kutoa Elimu endelevu kwa wakulima pamoja na kuwawezesha mbegu bora ya ufuta kilo mbili 2 kwa kila mwanakikundi aliyeshiriki mafunzo hayo, kwa idadi ya wanachama 25 kwa kila kikundi.
Amewataka washiriki wa mafunzo hayo kuwa wasikivu na kufuata maelekezo yote yatakoyotolewa na wawezeshaji wa mafunzo hayo ili waweze kujiinua kipato kwa kuuza mazao yao kwa kutumia mfumo wa stakabadhi gharani kwa kupeleka mavuno yao kwenye chama cha Msingi cha WEST AMCOS kilichopo Manispaa ya Songea ili kuondoa unyonyaji kwa wakulima.
Naye Afisa kilimo kata ya Matogoro Salumu Mkwamba alibainisha kuwa zao la ufuta ni zao la biashara ambalo mbegu zake zina kiasi kikubwa cha mafuta kiasi cha asilimia 45% hadi asilimia 55% ambapo mafuta ya ufuta yanathamani kubwa hivyo hulifanya kuwa zao bora la biashara.
Zao la ufuta hustawi katika maeneo yenye udongo mwepesi mweusi na usio tuamisha maji na udongo tifu tifu ambapo aliongeza kuwa mbegu za asili zina uwezo wa kutoa mavuno kidogo na huchukua siku 140 hadi 180 kukomaa na hutoa mavuno kati ya kilo 150 hadi 300, na ikiwa utatumia mbegu za kisasa zinauwezo wa kukomaa kwa muda mfupi na hutoa mavuno mengi kwa wastani wa kilo 500-1000 lakini hutegemeana na huduma. “ Alibainisha Mkwamba”
Akiitaja aina za mbegu za kisasa ni pamoja na naliendele 92, Lindi 202, Ziada 94, Mtwara, Lindi White, na Naliendele 2002. Zao la ufuta kwa Tanzania hulimwa mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Manyara, Pwani, Singida na Tanga. Nk.
IMETAYARISHWA NA;
AMINA PILLY;
AFISA HABARI MANISPAA YA SONGEA.
24.11.2020
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa