MANISPAA YA SONGEA YAVUNJA MKATABA NA LUKOLO
HATIMAYE Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma imevunja rasmi Mkataba wa ujenzi wa lami nzito kati yake na Kampuni ya Lukolo yenye makao makuu yake Jijini Dar es salaam.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Eng.Samwel Sanya amesema muda wa Mkataba wa kumaliza kazi kwa Mkandarasi huyo ulimalizika tangu Juni 30 mwaka huu.
Amesema baada ya muda huo kumalizika Mkandarasi huyo aliingizwa kwenye tozo(Liquidated Damage) na kwamba iwapo atashindwa kumaliza kazi kwa siku 100 hatua za kisheria za kuvunja mkataba zitafanyika.
“Oktoba 8,2017 ndiyo siku 100 alizopewa Mkandarasi huyo zimemalizika hivyo tumevunja mkataba rasmi na Mkandarasi huyo,amekatwa asilimia 10 ambayo ni sawa na sh.bilioni 1.4 kwa kuchelewesha mradi na anatakiwa kulipa asilimia 15 ya fedha kwa kazi ambazo hajamaliza ndani ya mkataba’’,anasisitiza Sanya.
Mkandarasi huyo pia anatakiwa kurudisha kiasi cha shilingi bilioni 2.15 kiasi cha fedha ambacho kilitolewa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB),fedha ambazo zilitolewa kwa ajili ya kusafirishia mitambo mbalimbali ya ujenzi katika mradi huo.
Kaimu Mkurugenzi huyo wa Manispaa ya Songea amesema baada ya kuvunjwa mkataba huo,Manispaa inaanza mchakato wa kumtafuta Mkandarasi mwingine ili kuendeleza kazi ya ujenzi wa barabara na kwamba Manispaa haijapata hasara yeyote baada ya kuvunjwa kwa mkataba huo.
Zaidi ya sh.bilioni 14 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi wa barabara za Mji wa Songea katika kiwango cha lami nzito zenye urefu wa kilometa 8.6.
Fedha za mradi huo zimetolewa na Benki ya Dunia chini ya Mpango wa kuzijengea uwezo serikali za mitaa(ULGSP), mpango huo unakusudia kuendeleza miundombinu ya Halmashauri za miji na Manispaa 18 za Tanzania Bara ikiwemo Manispaa ya Songea.
Mradi huo ambao ulianza Juni Mosi 2015 ulitarajiwa kukamilika Juni 30,2017 ambapo fedha iliyopokelewa na Manispaa ni zaidi ya sh.bilioni saba ambapo hadi sasa Mkandarasi ameshalipwa zaidi ya sh.bilioni nne.
Barabara za Manispaa ya Songea ambazo zipo kwenye mradi huu ni FFU hadi Matogoro yenye urefu wa kilometa 3.2,barabara ya Songea Girl’s hadi Mateka yenye urefu wa kilometa 1.5 na barabara ya Mwembechai hadi Bombambili yenye urefu wa kilometa 2.6.
Barabara nyingine ni Mitumbani hadi Yapenda yenye urefu wa kilometa moja,barabara ya Polisi hadi Stendi ya Mlilayoyo yenye urefu wa kilometa 0.45.
Taarifa imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa