HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea imekabidhi rasmi mradi wa maji kwa Jumuiya ya Watumia Maji wa Ruhuwiko Kanisani(RUHUWASO),ambao ulifadhiliwa na Benki ya Dunia kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 429.65
Makabidhiano ya mradi huo yamefanyika Mei 5,2018 katika ofisi za Mtaa wa Ruhuwiko Kanisani na kuhudhuriwa na wananchi wa Mtaa huo wakiongozwa na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa na Diwani wa Kata na viongozi wa RUHUWASO.
Akizungumza kabla ya kukabidhi mradi huo,Mhandisi wa Maji Manispaa ya Songea Mhandisi Samwel Sanya amesema mradi huo umekabidhiwa kwa RUHUWASO ili waweze kuutunza,kuulinda na kuuendesha bila kuitegemea Halmashauri na kwamba Halmashauri itaendelea kutoa huduma za ushauri na kitalaam.
Hata hivyo mara baada ya Manispaa kukabidhi mradi huo kwa RUHUWASO nao waliukabidhi kwa Mamlaka ya Maji Safi Songea(SOUWASA) ambao kulingana na sheria SOUWASA wana mamlaka ya kuingiza maji ndani ya nyumba.
“Kwa sababu Mtaa wa Ruhuwiko kanisani upo ndani ya mji na sio pembezoni na wananchi wengi wanahitaji kuingiziwa maji ndani hivyo wananchi wameamua jambo la busara kukabidhiwa mradi kwa SOUWASA’’,anasisitiza Mhandisi Sanya.
Halmashauri ya Manispaa ya Songea imekabidhi mradi huo kwa RUHUWASO ukiwa na vyanzo viwili vya maji vilivyo chini ya ardhi,nyumba mbili za mitambo,birika la kuhifadhia maji lenye ujazo wa lita 135,000,mtandao wa maji wenye urefu wa kilometa tisa,vituo 16 vya kuchotea maji,birika tatu za uvunaji wa maji ya mvua na vyumba 25 vya vigawo vya maji.
Mradi wa maji katika Mtaa wa Ruhuwiko Kanisani, uliibuliwa na Wananchi wenyewe mwaka wa fedha 2013/2014 na kuanza kujengwa mwaka wa fedha 2014/2015,Mkandarasi akiwa ni Girafe Investment Company.
Watu wapatao 3,447 kutoka katika Mtaa wa Ruhuwiko Kanisani wanatarajia kunufaika na mradi huo wa maji safi na salama baada ya mradi kukamilika,
Imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Mei 6,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa