HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma katika kipindi cha Julai 2017 hadi Juni 2018 imefanikiwa kuteketeza bidhaa zilizoharibika,kupitwa muda wa matumizi na vipodozi vyenye viambata vyenye sumu vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni tisa.
Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Manispaa ya Songea Dkt.Mameritha Basike,kati ya bidhaa hizo ni vipodozi vya kawaida vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni tano,vipodozi vya sumu vyenye thamani ya shilingi milioni 1.9 na vyakula vyenye thamani ya shilingi milioni 2.16.Amesema bidhaa hizo zilikamatwa katika ukaguzi wa kawaida ambao umekuwa unafanyika katika kipindi cha kuanzia Julai 2017 hadi Juni 2018 katika Kata mbalimbali za Manispaa ya Songea.
Akizungumzia Huduma za afya ya uzazi na mtoto ,Dkt.Basike amesema katika kipindi hicho zimeendelea kutolewa katika vituo 30 vya Manispaa ya Songea na kwamba katika kipindi hicho jumla ya akinamama wajawazito waliotarajiwa ni 9024,hata hivyo jumla ya akinamama wajawazitio 16,366 sawa na asilimia 181.4 walihudhuria kliniki.
Amesema kati yao akinamama wajawazito 6,436 walipimwa ugonjwa wa kaswende kati yao akinamama 71 sawa na asilimia 1.1 waligudulika kuwa na kaswende na walipewa matibabu pamoja na wenzi wao.Kulingana na Mganga Mkuu wa Manispaa ya Songea katika kipindi hicho akinamama 9,024 walitarajiwa kujifungua badala yake jumla ya akinamama 11,078 sawa na asilimia 122.8 walijifungua.
Basike amebainisha zaidi kuwa katika kipindi hicho jumla ya watoto 10,524 walitarajiwa kuzaliwa,badala yake watoto 10,340 sawa na asilimia 98.3 walizaliwa na kwamba watoto waliozaliwa wafu katika kipindi hicho walikuwa ni 175 sawa na asilimia 1.7.Hata hivyo amesema katika kipindi hicho jumla ya akinamama waliotumia uzazi wa mpango ni 17,674 sawa na asilimia 63.1
Imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Agosti 7,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa