MAPOROMOKO ya Kalambo yaliopo kijiji cha Kapozwa,kata ya Kisumba wilayani Kalambo mkoani Rukwa yanatokana na mto Kalambo ambao ni mpaka wa Tanzania na Zambia.Maporomoko ya maji haya ukiachilia kuwa ni ya pili baada ya yale ya Tugela Afrika ya Kusini lakini pia ndiyo maporomoko pekee yanayogawa mpaka wa nchi mbili za Tanzania na Zambia.
Maporomoko haya yamekuwa yakionekana na kutangazwa kuwa yapo Zambia na hivyo kuiondoa Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye maporomoko yanayotambulika duniani.Katika kijiji cha Kapozwa ambacho pia kilianzishwa kutokana na imani kuwa ukienda kuoga katika maporomoko hayo utapooza. Kwa kuambiwa hivyo wananchi wenyeji wa eneo hilo walipaita kijiji jina la kapozwa.
Maporomoko ya Kalambo yana kina cha mita zaidi ya 200 na yanatiririsha maji yake katika eneo la urefu wa kilomita tano kabla ya kuingia Ziwa Tanganyika katika kijiji cha Kipwa.
Awali ilidhaniwa kwamba kina cha maporomoko ya Mto Kalambo ni zaidi ya mita 300 lakini baada ya kupimwa na watalaamu miaka ya 1920 inakadiriwa kuwa kina chake ni zaidi ya mita 200. Vipimo vya mwaka 1956 vimetoa matokeo yanayoonesha kuwa yana kina cha mita 221 na upana wake ni kati ya mita 3.6 na 18.
Wataalamu wa malikale wanayaelezea maporomoko ya Mto Kalambo kuwa ni eneo lenye umuhimu wa kipekee barani Afrika na kwamba ni hazina kubwa ya kihistoria ikiwa na ushuhuda wa shughuli kadhaa zilizokuwa zikifanywa na binadamu katika eneo hilo zaidi ya miaka 250,000 iliyopita.Baadhi ya mabaki yenye vielelezo vya kihistoria yalifukuliwa mwaka 1953 na Mvumbuzi John Desmond katika eneo hilo.
Makala imeandaliwa na Albano Midelo
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa