WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema hakuna kahawa itakayoruhusiwa kuuzwa nje ya nchi kabla ya kukobolewa, kwa lengo la kuiongezea thamani kabla ya kuingizwa sokoni.
Pia, Waziri Mkuu ameziagiza halmashauri zinazolima kahawa nchini kuwa na kitalu chenye miche zaidi ya laki mbili ifikapo mwisho wa mwezi wa pili mwaka huu.“Wakati utakapofika uongozi wa Wizara ya Kilimo utakwenda kukagua iwapo agizo hili limetekelezwa’’.
Aliyasema hayo wakati akizungumza na wadau wa kahawa wa mkoa wa Ruvuma kwenye ukumbi wa Jimboni wilayani Mbinga.Waziri Mkuu alisema kuanzia sasa kahawa yote itakayozalishwa nchini ni lazima iongezewe thamani na hakuna kahawa yenye maganda itakayoruhusiwa kuuzwa nje ya nchi.
“Hairuhusiwi kutoa kahawa nchini na kuiuza nje ya nchi ikiwa bado na maganda, ni lazima iongezewe thamani ndipo ipelekwe katika masoko ya nje ya nchi ili iuzwe kwa bei nzuri.
Hatua hii itasaidia kuongeza mnyororo wa thamani na kusaidia kulinda uwekezaji wa viwanda uliofanyika nchini’’
Akizungumzia kuhusu madeni ya wakulima, aliagiza watendaji wote wa AMCOS waliohusika watafutwe na walipe deni. “Kwa sasa Serikali haina taratibu za kununua madeni ya chama chochote cha ushirika. Kuendelea na utaratibu huo kunachochea viongozi wa ushirika kufuja mali za ushirika. Lazima watambue ukifuja fedha za wanaushirika , Serikali iko na wewe.”
Alisema Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli haitorudi nyuma katika msimamo wake wa kuwasimamia wakulima nchini ili nao waweze kunufaika na kazi kubwa wanazofanya.Kadhalika, Waziri Mkuu aliwaagiza viongozi wa AMCOS wahakikishe wakulima wote wanasajiliwa na taarifa zao ikiwemo ukubwa wa mashamba,kiasi cha uzalishaji na mahali walipo zinatunzwa vizuri katika kompyuta.
Pia, Waziri Mkuu alimuagiza Mrajisi Msaidizi wa Mkoa wa Ruvuma akague AMCOS zote na kujiridhisha kama ziko hai na kwenye tatizo la uongozi aitishe uchaguzi.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu alisema minada yote ya kahawa itafanyika kwenye maeneo yanayolima ambayo yamegawanywa kwa kanda 1.Moshi (Kilimanjaro,Arusha,Tanga,Manyara) 2. Kagera ( Kigoma, Geita, Kagera, Mara) 3. Songwe ( Rukwa,Mbeya,Iringa,Katavi), na Mkoa wa Ruvuma utafanyika Mbinga
Alisema lengo ya kufanya minada hiyo katika maeneo yanayolima kahawa ni kuongeza uwazi katika biashara hiyo na kuwawezesha wakulima kujua bei ya mnada na kulipwa kwa wakati. Mkulima anaruhusiwa kupeleka kahawa katika mnada wowote nchini ilimradi azingatie sheria na taratibu husika
“Kila kanda inayolima kahawa nchini itakuwa na maeneo yake ya kuuzia kahawa na kahawa ya Mbinga itauzwa katika minada itakayofanyika Mbinga na bei kila mtu ataijua siku hiyo.”
Waziri Mkuu alisema Serikali imedhamiria kuimarisha kilimo cha zao la kahawa ili kila mmoja anayehusika na zao hilo akiwemo mkulima aweze kunufaika na kuongeza tija.
Kwa upande wao, wadau walifurahishwa na uamuzi wa Serikali wa kulisimamia zao kwa ukaribu na hasa baada ya kutangaza minada yote ya kahawa kufanyika katika maeneo yao na kwa uwazi.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa