NAIBU Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Josephat Sinkamba Kandege amekagua mradi wa barabara za kiwango cha lami katika manispaa ya Songea.
Akiwa katika barabara ya Tumbani-Yapenda,Kandege amemwagiza Mkandarasi huyo kuhakikisha kuwa barabara hiyo inawekwa lami kabla ya mvua kuanza.
“Manispaa ya Songea inaanza kupata mvua kuanzia Novemba hivyo mjitahidi kuhakikisha barabara hiyo inawekwa lami kabla ya Novemba ili pasiwe na kisingizio cha mvua kukwamisha kazi’’,anasisitiza Kandege.
Mkandarasi amemuahidi Naibu Waziri kuwa wamejipanga na watahakikisha kuwa barabara hiyo inawekwa lami nzito kabla ya mvua kuanza na kwamba katika kipindi cha mvua inakuwa vigumu kuweka lami.
Kampuni ya kimataifa ya serikali ya China inayoitwa China Sichuan International Co-operation (SIETCO) Machi 25 mwaka huu inaanza rasmi ukarabati wa barabara za Manispaa ya Songea kwa kiwango cha lami nzito.
Mkataba unaonesha kuwa ukarabati wa barabara hizo zenye urefu wa kilometa 10.3 unaanza Machi 25,2018 na unatarajia kukamilika Septemba 30,2019.
“Mkataba ni wa miezi 18,fedha ambazo zinatumika katika ukarabati huo ni bilioni 10.96,Mkandarasi wa sasa anaongeza kilometa zaidi ya mbili,pia ataweka taa za barabarani’’,amesema Mhandisi Niclous Danda.
Halmashauri ya Manispaa ya Songea ilivunja Mkataba wa ujenzi wa lami nzito yenye urefu wa kilometa 8.6 kati yake na Kampuni ya Lukolo yenye makao makuu yake Jijini Dar es salaam,baada ya Kampuni hiyo kukiuka masharti ya mkataba wa miaka miwili uliomalizika Juni 30 mwaka 2017.
Baada ya muda huo kumalizika Mkandarasi huyo aliingizwa kwenye tozo(Liquidated Damage) kwa siku 100 ambapo Oktoba 8,2017 ndiyo siku 100 alizopewa Mkandarasi huyo zilimalizika hivyoManispaa ilivunja mkataba rasmi na Kampuni ya Lukolo.
Fedha za mradi huo ambazo ni zaidi ya shilingi bilioni 14 zimetolewa na Benki ya Dunia chini ya Mpango wa kuzijengea uwezo serikali za mitaa(ULGSP), mpango huo unakusudia kuendeleza miundombinu ya Halmashauri za miji na Manispaa 18 za Tanzania Bara ikiwemo Manispaa ya Songea.
Mradi huo ambao ulianza Juni Mosi 2015 ulitarajiwa kukamilika Juni 30,2017.Barabara za Manispaa ya Songea ambazo zipo kwenye mradi huu ni FFU hadi Matogoro yenye urefu wa kilometa 3.2,barabara ya Songea Girl’s hadi Mateka yenye urefu wa kilometa 1.5 na barabara ya Mwembechai hadi Bombambili yenye urefu wa kilometa 2.6.
Barabara nyingine ni Mitumbani hadi Yapenda yenye urefu wa kilometa moja,barabara ya Polisi hadi Stendi ya Mlilayoyo yenye urefu wa kilometa 0.45.
Imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa