HATIMAYE Kampuni ya kimataifa ya China inayoitwa China Sichuan International Co-operation ndiyo imeshinda tuzo ya Zabuni ya kuendelea na ujenzi wa barabara za Manispaa ya Songea kwa kiwango cha lami nzito.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Tina Sekambo amesema Kampuni hiyo inatarajia kuanza mara baada ya kusaini mkataba baina ya Kampuni hiyo na Halmashauri ya Manispaa ya Songea.
Halmashauri ya Manispaa ya Songea ilivunja Mkataba wa ujenzi wa lami nzito yenye urefu wa kilometa 8.6 kati yake na Kampuni ya Lukolo yenye makao makuu yake Jijini Dar es salaam,baada ya Kampuni hiyo kukiuka masharti ya mkataba wa miaka miwili uliomalizika Juni 30 mwaka 2017.
Baada ya muda huo kumalizika Mkandarasi huyo aliingizwa kwenye tozo(Liquidated Damage) kwa siku 100 ambapo Oktoba 8,2017 ndiyo siku 100 alizopewa Mkandarasi huyo zilimalizika hivyoManispaa ilivunja mkataba rasmi na Kampuni ya Lukolo.
Baada ya kuvunjwa mkataba huo,Manispaa ya Songea ilianza mchakato wa kumtafuta Mkandarasi mwingine ambapo amepatikana Mkandarasi wa Kampuni ya China Sichuan International ambaye ataendeleza kazi ya ujenzi wa barabara na kwamba Manispaa haijapata hasara yeyote baada ya kuvunjwa kwa mkataba wa Mkandarasi wa kwanza.
Fedha za mradi huo ambazo ni zaidi ya shilingi bilioni 14 zimetolewa na Benki ya Dunia chini ya Mpango wa kuzijengea uwezo serikali za mitaa(ULGSP), mpango huo unakusudia kuendeleza miundombinu ya Halmashauri za miji na Manispaa 18 za Tanzania Bara ikiwemo Manispaa ya Songea.
Mradi huo ambao ulianza Juni Mosi 2015 ulitarajiwa kukamilika Juni 30,2017.Barabara za Manispaa ya Songea ambazo zipo kwenye mradi huu ni FFU hadi Matogoro yenye urefu wa kilometa 3.2,barabara ya Songea Girl’s hadi Mateka yenye urefu wa kilometa 1.5 na barabara ya Mwembechai hadi Bombambili yenye urefu wa kilometa 2.6.
Barabara nyingine ni Mitumbani hadi Yapenda yenye urefu wa kilometa moja,barabara ya Polisi hadi Stendi ya Mlilayoyo yenye urefu wa kilometa 0.45.
Taarifa imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa