HIVI karibuni Rais wetu Dkt.John Magufuli amemzawadia kiasi cha shilingi milioni 100 Mzee Jumanne Ngoma aliyegundua madini ya Tanzanite mwaka 1967 katika eneo la Mirerani mkoani Manyara.
Tunampongeza sana Rais wetu kwa kuwatambua watanzania ambao wameonesha uzalendo katika nchi yao kwa kuvumbua,kugundua na kuzilinda rasilimali za nchi ambazo zinatakiwa kuwanufaisha watanzania wote.
Mzee Benedict Mapunda (Rasha) mwenye umri wa miaka 66 mkazi wa kijiji cha Ntunduwaro ndiye aliyegundua kuteketea kwa moto kwa mgodi wa madini ya makaa ya mawe Ngaka uliopo Wilaya ya Mbinga Mkoa wa Ruvuma mwaka 2006.
Inakadiriwa moto huo uliwaka kwa miaka mitatu kuanzia mwaka 2003 hadi mwaka 2006 uliteketeza tani milioni sita za makaa ya mawe.Inaaminika Moto huo ulianza kuwaka tangu Septemba mwaka 2003.Moto huo usingegundulika mapema ungeweza kuteketeza mamilioni ya tani za makaa ya mawe.
Mzee Rasha anasema katika kipindi chote cha miezi mitatu cha kuzima moto huo alikuwa anasimamia kuhakikisha moto huo unazima kazi ambayo anasema aliifanya kwa uzalendo bila kulipwa kitu chochote na kwamba watalaam baada ya kuchimba na kuweka mchanga,waliondoka na kazi ya uangalizi hadi moto ulipozima mwaka 2006 aliachiwa pekee yake.
Hata hivyo uchunguzi,umebaini Mzee Rasha bado hajatambulika kwa kuokoa rasilimali adimu ya madini ya makaa ya mawe kwa nchi yake ambayo yalikuwa yanateketea kwa moto ardhini kwa miaka kadhaa.Rasha anafanyakazi ambayo haifanani na umri wake katika Kampuni ya TANCOAL kwenye mgodi wa Ngaka.
Mgodi huo hivi sasa unaingiza mabilioni ya fedha kwa Kampuni binafsi ya uchimbaji wa madini hayo ya TANCOAL na serikali inalipwa kodi na ushuru kutokana na kazi ya uchimbaji na usafirishaji wa madini hayo ilioanza tangu mwaka 2011.
Kaimu Meneja Mgodi wa Makaa ya mawe Ngaka Edward Mwanga anasema Kampuni ya TANCOAL inatambua mchango wa Rasha kuanzia alipogundua moto wakati unaunguza mgodi,mchango wake katika utafiti na sasa uchimbaji wa makaa ya mawe ndiyo maana hadi sasa licha ya kuwa na miaka 66 bado Kampuni imeamua kuendelea kumwajiri na kumtumia.
Utafiti uliofanywa Mwaka 2001,kwenye mgodi wa Ngaka ulibaini kuwepo kwa madini ya makaa ya mawe yanayoongoza kwa ubora duniani kiasi cha tani milioni 400 ambazo zinatarajiwa kuchimbwa kwa zaidi ya miaka 50.
Imeandaliwa na Albano Midelo
Afisa Habari Manipaa ya Songea
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa