Mheshimiwa Diwani wa Kata ya Mjimwema Sylivester Mhagama amefanya ziara ya siku tano katika kata yake yenye jumla ya mitaa mitano kwa ajili ya kusikiliza na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi wa kata yake hususani miundombinu ya barabara.
Ziara hiyo ilianza kufanyika tarehe 07/06/2021 na kuhitimishwa tarehe 11/06/2021 katika uwanja wa ofisi ya kata ya Mjimwema, akiwa ameambatana na Meneja wa Wakala wa barabara za mjini na vijijini (TARURA) Manispaa ya Songea Daudi Sweke ambaye ametumia ziara hiyo kwa kutoa elimu kwa wananchi kwa lengo la kuwajengea uelewa wakutosha wananchi kuhusiana na majukumu ya TARURA pamoja na kupokea changamoto mbalimbali zinazojitokeza kwa wananchi kuhusiana na miundombinu ya barabara.
Akizungumza wakati wa kikao hicho Meneja wa TARURA Manispaa ya Songea Daudi Sweke amesema kwamba jukumu lao kubwa ni kuhakikisha wanaboresha miundombinu ya barabara katika eneo la Manispaa ili wananchi waweze kuepuka na changamoto zinazojitokeza katika utoaji wa huduma za usafiri hasa katika kipindi cha masika kutokana na ubovu wa miundombinu.
Sekwe amewataka wananchi kuacha kutupa taka kwenye mifereji ya barabara za mitaa pamoja na kupanda miti kwenye maeneo ya barabara ili kuepuka usumbufu unaojitokeza wakati unapofanyika uboreshaji wa barabara hizo kwa kuongezeka gharama kwa ajili ya kung’oa visiki vya miti iliyopandwa.
Aidha ametoa rai kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa wakandarasi mara wanapotengeneza miundombinu ya barabara ili kuondoa malalamiko au migogoro ambayo inaweza kukwamisha wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo.pia amehaidi kufikia tarehe 30 ya mwezi Julai 2021 barabara zote zenye changamoto ambazo zimewasilishwa TARURA na Mheshimiwa Diwani Mhagama kata ya Mjimwema zitakuwa zimetengenezwa.’ Sekwe alieleza’
Katika kuhakikisha anafanya miradi mbalimbali ya maendeleo katika kata yake Mheshimiwa Diwani Mhagama ameandaa ligi ya mchezo wa mpira wa miguu kwaajili ya vijana wa Kata ya Mijmwema ‘Diwani Cup’ iliyozinduliwa rasmi na Mheshimiwa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Michael Mbano huku mshindi wa kwanza akipewa zawadi ya Tshs. 200,000 pamoja na zawadi mbalimbali kwa mchezaji bora, golikipa bora na mfungaji bora.
IMEANDALIWA NA,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA,
13.07.2021.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa