MILIONI 150 KUKARABATI SHULE YA WASIOONA
HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma imepokea zaidi ya sh.milioni 151 toka TAMISEMI kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa shule ya msingi ya wasioona Luhira.
Mradi huo unahusisha ujenzi wa mabweni matatu,vyoo vya ndani ya mabweni hayo vya matundu 18,shimo la choo na ukarabati wa darasa moja na kuezeka madarasa mawili.
Mradi huo ambao mkandarasi wake ni Wakala wa Majengo Tanzania(Tanzania Buldings Agency) ulianza Aprili 20,2017 na unatarajia kumalizika Oktoba 20 mwaka huu.
Shule ya msingi Luhira ina wanafunzi mchanganyiko wanaoona na wasioona.Kulingana na mwalimu mkuu msaidizi wa shule hiyo Gisbert Ndunguru jumla ya wanafunzi wanaoona ni 1411 kati yao wasichana 672 na wanaume 739.
Shule hiyo ina kitengo ajili ya watoto wasioona nchini ambacho kilianzishwa mwaka 1982,hata hivyo shule ya msingi Luhira ni miongoni mwa shule kongwe nchini ilianzishwa mwaka 1929,Waziri Mkuu wa kwanza wa Tanzania hayati Rashid Kawawa amepata elimu yake ya msingi katika shule hiyo.
Mkuu wa kitengo cha wanafunzi wasioona Luhira ambaye pia ni mlemavu wa macho Salum Hapendeki anasema kitengo hicho kina wanafunzi 44 wasioona kati yao wavulana ni 19 na wasichana ni 25 na kwamba uwezo wa kitengo hicho ni kuchukua wanafunzi wasioona 60.
Afisa Elimu Maalum katika Manispaa ya Songea Rehema Nyagawa anasema shule hiyo kwa muda mrefu imekuwa inakabiliwa na upungufu wa matundu ya vyoo hali ambayo inasababisha watoto wa kiume kujisaidia choo kimoja na walimu,shule ina majengo chakavu ambayo ni mabweni,jiko na bwalo la chakula na uchakavu wa magodoro na vitanda.
Hata hivyo Nyagawa anaipongeza serikali kwa mradi wa mabweni na matundu ya vyoo ambao utapunguza changamoto hiyo ambayo ilikuwa kero kwa wanafunzi wasioona na kuathiri taaluma.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa