Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini Dkt. Damas Ndumbaro Waziri wa Maliasili na Utalii ametoa fedha kiasi cha shilingi Milioni kumi na moja na laki tano kwa vikundi 17 ndani ya Halmashauri ya Songea kwa lengo la kuinua vikundi vya wajasiriamali ili kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili katika wanavikundi hao.
Zoezi hilo limefanyika leo tarehe 28 Mei 2021 katika ukumbi wa Manispaa ya Songea na kusimamiwa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Michael Mbano ambaye alikuwa akimwakilisha Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini Dkt. Damas Ndumbaro Waziri wa Maliasili na Utalii.
Mbano alisema Manispaa ya Songea ina jumla ya vikundi 21 vya wajasiliamali kati ya hivyo vikundi 17 vimewezeshwa kupata mkopo, na vikundi 4 havikukidhi vigezo vinavyokubalika.
Amewataka wajasiriamali waliopokea fedha hizo kuhakikisha wanazitumia matumizi sahihi ili waweze kutatua changamoto zinazowakabili ikiwemo na kukamilisha miradi iliyoanza kufanyika katika vikundi vyao na kuwasaidia kujikwamua kiuchumi wao binafsi na kuleta maendeleo kwenye jamii inayowazunguka. ‘Mbano alisisitiza’.
Naye Mratibu wa vikundi ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini Alela Yazidu Kapinga amesema jumla ya vikundi 17 vyenye jumla ya wanachama 417 wamepokea fedha kutoka kwa Mbunge wa Songea Mjini yenye jumla ya thamani ya shilingi milioni kumi na moja na laki tano kwa wajasiliamali wanaojishughulisha na miradi mbalimbali ikiwemo utengenezaji wa bidhaa za sabuni, ufugaji wa kuku na kilimo.
Kwa nyakati tofauti wakitoa shukrani za dhati wajasiriamali hao “walisema wanashukuru kwa msaada uliotolewa na Mbunge Dkt. Damas Ndumbaro ambapo wameahidi kuendeleza miradi ya vikundi kwa kuwezeshana pamoja na kubuni miradi mingine mipya yenye tija kwa ajili ya ustawi wa vikundi vyao.”
Fedha hizo hazijatolewa kama mkopo na hazina riba, kwa lengo mahususi la kuwainua wajasiliamali wadogo wadogo waishio Songea Mjini.
IMEANDALIWA NA,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA YA SONGEA,
28.05.2021.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa