NA,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
22.10.2021
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Balozi Wilbert Ibuge ameongoza kikao cha Tathimini ya utekelezaji wa mpango wa jamii shirikishi na harakishi wa utoaji chanjo ya UVIKO 19 katika Mkoa wa Ruvuma, kikao ambacho kimefanyika leo tarehe 22 Oktoba 2021 katika ukumbi wa Manispaa ya Songea na kuhudhuriwa na wakuu wa Wilaya zote, wakurugenzi wa Halmashauri zote, viongozi mbalimbali pamoja na wataalamu wa afya.
Akizungumza katika kikao hicho Ibuge amewapongeza wajumbe wa kamati ya afya ya Mkoa kwa kuelimisha na kuhamasisha jamii kupata chanjo ya UVIKO 19 kwa hiari, na kufanikiwa kwa kiwango kikubwa katika utekelezaji wa mpango wa chanjo iliyotolewa kwa awamu ya kwanza Jassen&Jassen, ambapo wananchi wenye sifa ya kupata chanjo 44,549 sawa na asilimia 99% waliweza kupatiwa chanjo kati ya wananchi 45,020 waliotakiwa kupatiwa chanjo hiyo.
Aliongeza kuwa Serikali ya Tanzania imepokea chanjo aina ya Sino pharm dozi 1,065,600 kwa lengo la kusambaza katika maeneo yote nchini ambapo Mkoa wa Ruvuma umepokea dozi za Sino pharm 31,291 kwa ajili ya kuendelea na zoezi la kutoa chanjo kwa awamu ya pili.
Amewataka viongozi wa kila Halmashauri na wataalamu wa afya kuhakikisha wanatoa elimu na kuhamasisha jamii kushiriki kwa hiari katika zoezi la utoaji chanjo ya UVIKO 19 kwa awamu ya pili ambayo itaanza kutolewa rasmi kwenye vituo vya afya 298 vilivyopo Mkoani Ruvuma ifikapo tarehe 25 Oktoba 2021.
Pia kila Halmashauri inatakiwa kuhakikisha inasambaza chanjo za Sino pharm katika vituo vyote vinavyotoa chanjo za kawaida ambapo matarajio ya Mkoa ni kumaliza chanjo zilizopokelewa ndani ya siku 28 tangu tarehe 25 Oktoba 2021 ya kuanza zoezi hilo la utoaji chanjo hiyo.”Ibuge alisisitiza”
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mpango wa jamii shirikishi na harakishi wa utoaji wa chanjo ya UVIKO 19 kwa awamu ya kwanza Mratibu huduma za chanjo Mkoa wa Ruvuma Winbroad Mvile amesema kuwa utaratibu wa utoaji wa chanjo ya Sino pharm unatakiwa uzingatie njia zilizotumika katika utekelezaji wa utoaji chanjo ya awamu ya kwanza ili wananchi wengi Zaidi waweze kupata chanjo hiyo.
Alisema kuwa mlengwa wa chanjo ya Sino pharm ni mtu yeyote mwenye umri kuanzia miaka 18 ambapo atatakiwa kuchanjwa mara mbili ili mwili kupata kinga kamili dhidi ya UVIKO 19 ambapo amesisitiza wataalamu wa afya kutoa elimu hii kwa jamii ili kujenga uelewa juu ya matumizi sahihi ya chanjo ya Sino pharm.
Chanjo ya Sino pharm ni salama na ina uwezo wa kusisimua mwili ukatengeneza kinga dhidi ya UVIKO 19 kwa asilimia 95% iwapo mlengwa atakamilisha dozi mbili baada ya siku 21 hadi 28 tangu alipochanjwa dozi ya kwanza.”Mvile alibainisha”
Pia, ameeleza kuwa miongoni mwa faida ya chanjo ya UVIKO 19 ni pamoja na kusaidia kutengeneza kinga dhidi ya virusi vya SARS-CoV-2, kulinda mwili dhidi ya maradhi yanayosabaishwa na UVIKO 19 pamoja na kupunguza uwezekano wa kuenea kwa maambukizi ya ugonjwa huo.
Halmashauri ya Manispaa ya Songea imepokea chanjo ya UVIKO 19 aina ya Sino pharm dozi elfu tano na mia tatu (5300) ambazo zinatarajiwa kuanza kutolewa rasmi katika vituo vyote vya huduma ya afya vinavotoa chanjo nyingine ifikapo tarehe 25 Oktoba 2021.
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa