NA,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
26.10.2021.
Mkoa wa Ruvuma wajipanga kuanza rasmi utekelezaji wa kilimo cha pamoja/mkataba katika msimu wa mwaka 2021/2022 yaani (Block Farming).
Akizungumza katika kikao kilichofanyika leo tarehe 26 Oktoba 2021 katika ukumbi wa Manispaa ya Songea, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Balozi Wilbert Ibuge amesema kuwa lengo la kikao hicho ni kujadili muhstakabali wa maandalizi ya utekelezaji wa mkakati wa kilimo cha pamoja/mkataba Mkoani Ruvuma.
Ibuge alisema kuwa kilimo cha pamoja kinahusisha utengaji wa maeneo ambapo wakulima hulima katika eneo moja na kupata huduma za ugani kwa pamoja. Aidha, katika Halmashauri zote 8 Mkoani Ruvuma maeneo yaliyotambuliwa kwa ajili ya kilimo hicho ni jumla ya ekari 48,343.35 ambapo mahitaji ya Mbegu bora za mazao ya soya, ufuta, na alizeti ni tani 310.2 (soya tani 244.4, alizeti tani 35.2 na ufuta tani 30.59) pamoja na mahitaji ya mbolea ambayo ni tani 1,662.”Alibainisha”
Aliongeza kuwa kila mkulima anayo nafasi katika kushiriki kwenye utekelezaji wa kilimo cha pamoja au kilimo cha mkataba ambacho kinahusisha makubaliano baina ya mkulima na kampuni ambayo itahusika kutoa pembejeo, huduma za ugani pamoja na ununuzi wa mazao na kuzitaka Halmashauri zote kuhakikisha wanasimamia makubaliano hayo kwa lengo la kumlinda na kumnufaisha mkulima.’Alisisitiza’
“Utekelezaji wa kilimo cha pamoja/mkataba unahusisha mazao ya kimkakati ambayo ni alizeti, ufuta pamoja na soya ambapo kila Halmashauri inatakiwa kutenga eneo maalumu kwa ajili ya kutoa maelekezo na kufanya utafiti juu ya ubora wa mbegu za mazao ya mkakati” Ibuge alibainisha
Amezitaka kila Halmashauri kusimamia kikamilifu utekelezaji wa kilimo cha pamoja/mkataba kwa kutoa mafunzo kwa wakulima na maafisa ugani ili kujenga uelewa zaidi juu ya namna ya kulima kibiashara na kuongeza thamani ya kilimo ambapo mafunzo kwa maafisa ugani yanatarajiwa kufanyika ifikapo Novemba 2021.
Ametoa wito kwa wakulima wote Mkoani Ruvuma kuendelea na kilimo cha mazao ya chakula huku wakiendelea na kilimo cha pamoja/mkataba na kwa kufanya hivyo kutaongeza thamani ya kilimo katika Mkoa wa Ruvuma.”Alisisitiza”
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Songea Dkt Frederick Sagamiko alisema kuwa Manispaa ya Songea imefanikiwa kuhamasisha vikundi mbalimbali kushiriki katika kilimo cha pamoja/mkataba ikiwemo na vikundi vya wakulima wa soya kutoka Mwanamonga ambao watalima jumla ya ekari 163 na tayari wamesaidiwa kupata wadau mbalimbali watakaowapatia pembejeo zote za kilimo.
Alisema kuwa Halmashauri inaendelea kuhamasisha wadau na wakulima wenye maeneo makubwa kujitokeza ili waweze kushiriki kilimo cha pamoja/mkataba kwa kutoa elimu ya kilimo hicho kwa wananchi, vikundi, Sacoss na Amcos pamoja na kushirikiana na taasisi isiyo ya kiserikali ICODE na PASS kwa lengo la kuwajengea uwezo wakulima katika vikundi ili taasisi za kifedha ziweze kutoa mikopo ya kilimo.
Mashamba yaliyopendekezwa kulimwa Mkoani Ruvuma katika msimu 2021/2022 ni jumla ekari 12,570 na kati ya hizo ufuta ekari 5,279, soya ekari 3,856 na alizeti ekari 3,435, ambapo kwa Halmashauri ya Manispaa ya Songea maeneo yaliyotambuliwa ni Lilambo, Mletele na Tanga.
Mwisho
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa