Serikali imekuwa ikichukuwa juhudi mbalimbali katika kuhakikisha inatokomeza ukatili wa kijinsia katika jamii ikiwemo na kutunga sheria na miongozo mbalimbali inayotolewa na Serikali, pamoja na Juhudi hizo, bado kuna matukio mbalimbali yanayotokea katika jamii ambayo yanatakiwa kuzuia.
Hayo yamejiri wakati wa uzinduzi wa Maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili Mkoani Ruvuma yaliyofanyika tarehe 28 Novemba 2023 katika eneo la Soko kuu Songea iliyohudhuriwa na wadau mbalimbali, wananchi na viongozi kwa lengo la kujenga uelewa kuhusu ukatili wa kijinsia kama uvunjaji wa haki za binadamu kijamii, kiaifa, kikanda na kimataifa.
Akizungumza Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma Jeremia Sindoro ameitaka jamii kutumia vyombo vinavyohusika ikiwemo na madawati ya kijinsia, Ustawi wa jamii na vyombo katika kutokomeza matukio ya kikatili katika jamii.
Sindoro alisema Mkoa wa Ruvuma ni wa pili kitaifa kwa mimba za utotoni ikiwa ni 37% huku Mkoa wa Songwe ukiwa nafasi ya kwanza kwa mimba za utotoni ambapo amewataka wananchi kuwekeza maadili kwa kufanya mazungumzo na watoto ili kuhakikisha wanatimiza wajibu wao pamoja na ndoto zao sambamba na mafundisho ya dini.
Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya jamii Mkoa wa Ruvuma Mariamu Juma amesema lengo la maadhimisho hayo ni kuungana na wadau, kupata nguvu ya pamoja katika kuhimiza na kushawishi jamii kutokomeza vitendo vya kikatili wa kijinsia ili kufikia usawa wa kijinsia.
Bi Mariamu alibainisha malengo mahususi ni pamoja na kuonyesha mshikamno ulimwenguni kote juu ya kupinga vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake, na kuwaunganisha wadau kwa pamoja ili kuendelea kusisitiza wajibu wao katika kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Kauli mbiu ya mwaka 2023 ni “WEKEZA: KUZUIA UKATILI WA KIJINSIA.”
IMEANDALIWA NA;
AMINA PILLY
KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa