KATIBU Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Prof.Riziki Shemdoe amesema Mkoa wa Ruvuma umedhamiria kuhakikisha kuwa hadi kufikia mwaka 2020 pasiwepo na mwanafunzi hata mmoja asiyejua Kusoma, Kuandika na Kuhesaba(KKK).
Hayo yamesemwa katika hotuba ya Katibu Tawala huyo,iliyosomwa na Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Ruvuma Edmund Siame kwenye mafunzo ya kuibua na kubadilishana simulizi za mabadiliko,yalioshirikisha Halmashauri zote nane za mkoa wa Ruvuma na kufanyika kwenye ukumbi wa kanisa katoliki Jimbo la Mbinga.
Shemdoe amesisitiza kuwa kuwepo kwa wanafunzi wasiojua KKK ni jambo la aibu hivyo ameagiza kila mmoja awajibike katika nafasi yake ili kuhakikisha azima ya kupunguza na kumaliza changamoto ya KKK inatekelezwa kwa vitendo.
“Wanafunzi wasiojua KKK,waondolewa kwa sababu ni aibu atakwendaje mtoto sekondari bila kujua kusoma na kuandika yaani unakuwa umetengeneza kizungumkuti”,amesisitiza.
Ametoa rai kwa wadau waliopata mafunzo hayo kutengeneza mazingira ya wanafunzi kujua KKK wanapomaliza elimu ya msingi na kusisitiza kuwa ni jambo la ajabu mwanafunzi kumaliza darasa la saba akikosa stadi hizo muhimu.
Ameagiza kuwa serikali ya Mkoa wa Ruvuma inataka wanafunzi wanaomaliza darasa la pili wawe wanajua KKK na kwamba waingie darasa la tatu wakiwa wameimarika kitaaluma na kwamba iwapo mwanafunzi hajui KKK hasiruhusiwe kuendelea na darasa la tatu.
Kwa upande wake Mratibu wa Mpango wa TUSOME PAMOJA katika Mkoa wa Ruvuma Bwana Msabaha amesema hayo ni mafunzo ya awamu ya pili ya simulizi za mabadiliko ambapo katika awamu ya kwanza maafisa hao walipewa mafunzo ya namna ya kuandaa simulizi za mabadiliko.
Msabaha amesema mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa TUSOME PAMOJA katika maeneo matatu ikiwemo eneo la uboreshaji wa KKK,uboreshaji wa mfumo wa elimu na eneo la ushiriki wa jamii katika elimu.
Hata hivyo amesema Mpango wa TUSOME PAMOJA unakaribia kufikisha mwaka wa tatu wa utekelezaji wake na kwamba imebakia miaka miwili ya utekelezaji na kwamba kuna baadhi ya maeneo ya utekelezaji yamefanyika vizuri,na baadhi ya maeneo yapo katikati na maeneo mengine yapo chini.
“Simulizi za mabadiliko zitasaidia kuleta mabadiliko kutoka eneo moja ambalo utekelezaji haukufanyika vizuri hadi eneo jingine kwa kujifunza toka Halmashauri moja iliyofanya vizuri kwenda nyingine’’,amesisitiza Msabaha.
Mafunzo hayo yaliyoratibiwa na Mpango wa TUSOME PAMOJA yanayofanyika kwa siku mbili yanashirikisha maafisa elimu,maafisa habari,wenyeviti wa waratibu,maafisa maendeleo ya jamii na wanahabari.
TUSOME PAMOJA ni Mpango unaofadhiliwa na USAID ambao unafanyiwa majaribio katika mikoa ya Ruvuma,Iringa,Morogoro na Mtwara na unalenga kusaidia kuboresha stadi za ufundishaji na KKK katika shule za msingi.
Imeandaliwa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Desemba 8,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa