Na,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
25 JULAI 2022
Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Kamando Mgema amewaongoza wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kuadhimisha siku ya kumbukumbu ya mashujaa ambayo huadhimishwa kila mwaka ifikapo Julai 25.
Maadhimisho hayo yamefanyika nchi nzima kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii ambapo Mkoa wa Ruvuma umeadhimisha kwa kufanya usafi wa mazingira katika eneo la soko la Bombambili lililopo ndani ya Manispaa ya Songea.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Pololet alisema kuwa “Maadhimisho hayo ni kumbukumbu muhimu katika historia ya nchi ya Tanzania ambapo tunawaenzi mashujaa waliojitoa mhanga kupigania haki, uhuru na amani wa Taifa letu”.
Aliongeza kuwa Mkoa wa Ruvuma umeadhimisha siku hiyo kwa kufanya usafi pamoja na kutembelea eneo la Makumbusho lililopo Manispaa ya Songea katika makaburi ambayo walizikwa mashujaa waliopigana vita vya Majimaji mnamo mwaka 1906 – 1907.’Alibainisha’
Pololet ametoa rai kwa wananchi wote Mkoani Ruvuma kuendelea kulinda Amani ya Taifa la Tanzania pamoja na kuhakikisha wanatunza mazingira yanayowazunguka kwa kudumisha utaratibu uliowekwa na Serikali wa kufanya usafi kwenye maeneo mbalimbali ya umma kila ifikapo tarehe ya mwisho wa kila mwezi.
Naye Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro (MB) ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kuendelea kuenzi mashujaa hao kwa kudumisha uzalendo, umoja na mshikamano ili kuchochea amani ndani na nje ya mipaka ya Tanzania. ‘Alisisitiza’
Dkt. Ndumbaro amewataka wananchi wote kushiriki kikamilifu katika zoezi la sensa ya watu na makazi linalotarajiwa kufanyika ifikapo Agost 23 mwaka huu kwa lengo la kupata Takwimu sahihi zitakazosaidia Serikali kupanga mikakati ya kuleta maendeleo kwa wananchi.
Amewahamasisha wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kushiriki katika Tamasha la Majimaji Serebuka linaloendelea kufanyika katika uwanja wa Majimaji uliopo Manispaa ya Songea lenye lengo la kudumisha uzalendo pamoja na urithi wa utamaduni kupitia michezo mbalimbali.
Akizungumza wakati wa zoezi la kufanya usafi katika soko la Bombambili, Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Dkt. Frederick Sagamiko alisema kuwa Manispaa ya Songea imejipanga kuimarisha usafi wa mazingira kwa kuboresha mfumo wa uzoaji taka katika maeneo ya umma ikiwemo na masoko kwa kuanza kutoa mikopo ya usafiri aina ya Toyo kwa vikundi, ambao utatumika kwa ajili ya ukusanyaji wa taka hasa kwenye maeneo yasiyoweza kufikiwa na magari makubwa.
Dkt. Sagamiko ametoa wito kwa wananchi kuunda vikundi vya wajasiriamali kwa kuzingatia makundi maalum (wanawake, vijana na watu wenye ulemavu) ili kuweza kupata fursa za mikopo ambayo itasaidia kukuza uchumi binafsi pamoja na Taifa wa ujumla.
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa