Na,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
26.04.2022
Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Kamando Mgema ameongoza wakazi wa Manispaa ya Songea kwenye zoezi la usafi wa mazingira kwa kufanya usafi katika maeneo mbalimbali ikiwemo na eneo la soko kuu la Manispaa ya Songea pamoja, Soko la Manzese, pamoja na vituo vya afya.
Tukio hilo limefanyika kufuatia maadhimisho ya siku ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambayo huadhimishwa kila mwaka ifikapo mnamo tarehe 26, Aprili ambapo Mkoani Ruvuma siku hii imetumika katika kuchochea jamii kushiriki katika zoezi la usafi wa mazingira.
Akizungumza na wananchi baada ya zoezi la usafi, Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Kamando Mgema kwaniaba ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, “amesema kuwa katika maadhimisho haya Mkoa wa Ruvuma umelenga kuchochea uzalendo na utamaduni wa kufanya usafi wa mazingira uliowekwa na Serikali kila ifikapo jumamosi ya mwisho wa mwezi.”
Pololet amewataka wananchi kujenga tabia ya kufanya usafi wa mazingira yanayowazunguka kila siku kwa lengo la kujiepusha na magonjwa mbalimbali pamoja na kuweka Mkoa wa Ruvuma katika hali ya usafi.”Alisisitiza”
Alisema kuwa wajibu wa kuondoa takataka ni jukumu la watu wote ambapo kila mwananchi anatakiwa kushiriki kwa kufuata muongozo uliowekwa na Halmashauri ya Manispaa ya Songea kwa kuchangia gharama za uzoaji wa takataka kwa kila nyumba.
Ametoa maagizo kwa Afisa mazingira Manispaa ya Songea pamoja na viongozi wa masoko kuhakikisha kuwa kila siku kabla ya kuanza kufanya biashara wafanyabiashara wote waanze kwa kufanya usafi katika maeneo yao.
Aliongeza kuwa kila mwananchi anatakiwa kufanya usafi katika maeneo ya umma ifikapo jumamosi ya mwisho wa mwezi pamoja na kila jumamosi ya mwisho wa wiki kutumika kama siku ya kufanya mazoezi kwa lengo la kuimarisha afya.’Pololet alisisitiza’
Kwa upande wake Afisa Mazingira Manispaa ya Songea Philipo Benno Mpwesa alisema kuwa Manispaa ya Songea ilipokea agizo la kuadhimisha siku hii kwa kufanya usafi wa mazingira kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo zoezi hilo limefanyika katika kila mtaa yote 21 iliyopo ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Songea.
Naye Mstahiki Meya Manispaa ya Songea Michael Mbano alieleza kuwa Manispaa ya Songea imejipanga kukabiliana na changamoto ya ongezeko la uzalishwaji taka kwa kuimarisha mfumo wa uzoaji taka hizo ambapo hadi kufikia Julai 2022 Halmashauri itaweza kutoa fursa kwa Taasisi binafsi ili kusaidia kusafisha Manispaa ya Songea.
Amewataka kuanzia tarehe 27 Aprili 2022 kila mfanyabiashara mdogo (machinga) kuhakikisha anafanya biashara katika maeneo rasmi yaliyopangwa na Serikali kwa lengo la kuendelea kudhibiti uchafuzi wa mazingira unaotokana na ufanyaji biashara katika maeneo yasiyo rasmi na kukiukwa kwa agizo hilo hatua za kisheria zitachukuliwa. “Alisisitiza”
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa