Na,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
19 MEI 2022
Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Kamando Mgema amezindua zoezi la utoaji chanjo ya ugonjwa wa polio awamu ya pili kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano.
Uzinduzi huo umefanyika leo tarehe 19 Mei 2022 katika ukumbi wa Manispaa ya Songea na kuhudhuriwa na wakuu wa Wilaya zote Mkoani Ruvuma, wakurugenzi wa Halmashauri, wataalamu wa afya pamoja na viongozi mbalimbali.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mgema alisema kuwa lengo la utoaji wa chanjo hiyo ni kuongeza kinga ya kuzuia uwezekano wa watoto walio na umri chini ya miaka 5 kupata madhara yatokanayo na virusi vya polio ambapo Mkoani Ruvuma zoezi la utoaji chanjo hiyo limeanza Mei 18 hadi ifikapo Mei 21, 2022.
Amewataka wataalamu wa afya kuhakikisha watoto lengwa wote Mkoani Ruvuma wanapatiwa chanjo hiyo ambayo itatolewa nyumba kwa nyumba, kwenye vituo vya afya 316 Mkoani Ruvuma pamoja na maeneo yenye mikusanyiko ya watoto ikiwemo na mashuleni.
Mgema amewataka wakuu wa Wilaya pamoja na wakurugenzi wa Halmashauri zote kusimamia zoezi la iutoaji chanjo kwa ufanisi ili kuhakikisha watoto wote lengwa Mkoani Ruvuma wanapata chanjo hiyo.
Ametoa rai kwa viongozi wa dini wote kuhamasisha na kutoa elimu kwa jamii kupitia nyumba za ibada kuhusiana na umuhimu wa watoto kupata chanjo hiyo ambayo ni salama na haina madhara yoyote kwa afya ya mtoto .”Alisisitiza”
Naye Mratibu wa huduma za chanjo Mkoa wa Ruvuma Dkt. Winbroad D. Mvile alisema kuwa ugonjwa wa Polio unasababishwa na kirusi cha Polio ambacho huenezwa kwa kula chakula na kunywa maji yaliyochafuliwa na kinyesi cha mtu mwenye ugonjwa huo.
Aliongeza kuwa ugonjwa huo huathiri zaidi watoto wenye umri chini ya miaka 5 ambapo dalili za ugonjwa huo ni pamoja homa, maumivu ya mwili, kichwa na shingo hali inayopelekea kupooza kwa ghafla na hatimaye kifo.
Mvile aliongeza kuwa Mkoa wa Ruvuma umepokea jumla ya chanjo ya Polio Laki 354,000 ambapo kwa awamu ya kwanza ulipokea chanjo Laki 278,000 na kwa awamu ya pili umepokea chanjo Elfu 76000 ambazo zinatarajiwa kutolewa kwa watoto lengwa walio chini ya miaka mitano Laki 241,966 kwa Mkoa wote wa Ruvuma.
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa