Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Tina Sekambo ameongoza Maandamano ya siku ya wauguzi duniani yaliyofanyika katika kituo cha afya Mjimwema Manispaa ya Songea leo tarehe 12.05.2021.
Maadhimisho hayo yameambatana na utoaji wa kiapo kwa wauguzi, utoaji wa zawadi kwa wagonjwa waliolazwa Hosptalini hapo, ambapo katika maadhimisho hayo yameshirikisha wauguzi kutoka zahanati zote za Manispaa ya Songea, ngazi ya kliniki, na vituo vya afya kwa lengo la kukumbushana wajibu na majukumu ya wauguzi ili kuleta mabadiliko chanya katika afya ya jamii.
Sekambo alianza kwa kuwashukuru wauguzi wote kwa kujitolea kufanya kazi kwa weledi ikiwemo na kutoa huduma bora kwa jamii sambamba na kupunguza maambukizi mapya ya VVU na magonjwa mbalimbali yanayoambukizwa kwa njia ya hewa, kupunguza vifo vya akinamama wajawazito pamoja na watoto wachanga ambapo kwa mwaka 2020 kituo cha afya Mjimwema akinamama 4984 walijifungua salama.
Miongoni mwa changamoto ambazo ameahidi kuzifanyia kazi ni pamoja na ukosefu wa vitendea kazi, ukosefu wa gari la kubebea wagonjwa (AMBULANCE) wanapopata rufaa ya kwenda hospitali nyingine, upungufu wa wauguzi ambapo Manispaa ya Songea inapaswa kuwa na wauguzi 233 lakini hadi sasa kituo kina wauguzi 91 sawa na asilimia 39% hivyo kuna upiunguzfu wa wauguzi 142 sawa na asilimia 60%.
Amemuagiza Afisa utumishi Manispaa ya Songea kutembelea kituo cha afya Mjimwema kwa ajili ya kusikiliza kero na kutoa elimu kwa wauguzi kuhusiana na masuala ya kiutawala, utumishi na maslahi ya watumishi wa kada ya Afya ‘Sekambo alibainisha’.
Naye Afisa muuguzi msaidizi Manispaa ya Songea Rhoda Mtung’e ametoa ombi kwa serikali kuendelea kutoa ajira kwa wauguzi wanaohitimu ili kupunguza au kuziba pengo la upungufu wa wauguzi katika Manispaa ya Songea pamoja na kuongeza vitendea kazi vya kutosha katika vituo vya afya ambavyo vinaupungufu ili kusaidia kupunguza vifo na malalamiko kutoka kwa wateja.
Mtung’e alisema lengo la kutoa kiapo kwa wauguzi ni kufanya kazi kwa uadilifu ikiwemo na kutotoa siri za wagonjwa, kutotoa au kupokea rushwa pamoja na kuzingatia misingi na maadili ya uuguzi kwa jamii.
Kauli mbiu ya siku ya wauguzi duniani mwaka 2021 ni “WAUGUZI SAUTI INAYOONGOZA DIRA YA HUDUMA YA AFYA”.
IMEANDALIWA NA,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA,
12.05.2021.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa