Na; Amina Pilly
Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea, Wakili Bashir Muhoja, amekutana na watumishi wa kada ya afya katika kikao cha mwaka kilichofanyika katika ukumbi wa Songea Club.ambapo Kikao hicho kililenga kusikiliza kero na changamoto zinazowakabili watumishi wa sekta ya afya katika Manispaa ya Songea.
Katika hotuba yake, Wakili Muhoja aliwapongeza watumishi hao kwa kazi kubwa na ya kujitolea wanayoifanya katika vituo vya kutolea huduma za afya, licha ya changamoto ya uhaba wa watumishi. Ambapo aliwahimiza kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na kuzingatia misingi ya kazi, ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora.
Mkurugenzi pia alitoa wito kwa watumishi hao kuweka bajeti ya pamoja ya ununuzi wa vitendea kazi, hatua itakayosaidia kurahisisha upatikanaji wa vifaa kwa wakati na hivyo kuboresha utoaji wa huduma.
Aliahidi kuboresha miundombinu ya vituo vya afya katika manispaa hiyo, ikiwemo Hospitali ya Manispaa, Kituo cha Afya Mjimwema, Ruvuma, Msamala pamoja na kitengo cha Ustawi wa Jamii.
Katika kikao hicho, alielezea hali ya sekta ya afya katika Manispaa ya Songea ambapo hadi sasa kuna jumla ya watumishi 385 kati ya mahitaji ya watumishi 912, Aidha, kuna zahanati 42, kliniki 10, vituo vya afya 9 pamoja na hospitali moja ya manispaa hali hii imekuwa changamoto katika utoaji wa huduma hasa kutokana na upungufu wa watumishi katika vitengo mbalimbali.

Kwa upande wake, Afisa Yahaya kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) aliwahimiza watumishi wa afya kuepuka vitendo vya rushwa na kuzingatia maadili ya kazi. Alisisitiza kuwa mapambano dhidi ya rushwa ni jukumu la kila mmoja na kuwa watumishi wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu.
“Kuzuia rushwa ni jukumu langu na lako, tutimize majukumu yetu,” alisema Yahaya.

Kaimu Afisa Utumishi wa Manispaa ya Songea, Bi. Lilian Sanga, aliwahimiza watumishi kutoa huduma bila upendeleo, kuepuka vitendo vya rushwa na kuwa na nidhamu ya kazi. Aliwakumbusha kuwa huduma ya afya ni huduma nyeti inayohitaji uadilifu mkubwa.
Aidha, Meneja wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (PSSSF), Bw. Edwin Msavangwa, alitoa elimu kuhusu kazi za mfuko huo, ikiwemo kuwatambua wanachama, kukusanya michango yao, kuhifadhi na kuwalipa mafao kwa wakati.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na viongozi wa vyama vya wafanyakazi kutoka TUGHE na TALGWU, pamoja na wanasaikolojia waliotoa elimu kuhusu afya ya akili. Washiriki walipata nafasi ya kuuliza maswali na kutoa maoni yao kuhusu namna bora ya kuboresha huduma za afya ndani ya Manispaa ya Songea.
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa