Na; Amina Pilly;
Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea, Wakili Bashir Muhoja, leo tarehe 15 Julai 2025 amekabidhi rasmi eneo la mradi wa ujenzi wa Soko la Kisasa katika maeneo ya Manzese A & B pamoja na kiwanda cha kuchakata mazao ya nafaka kilichopo Kata ya Lilambo kwa Mhandisi kutoka Kampuni ya China National Aero Technology International Engineering Cooperation.
Picha ya eneo la Soko la Manzese A kabla ya kuanza ujenzi.
Picha ya Eneo la Soko la Manzese B kabla ya kuanza ujenzi.
Mradi huo mkubwa unaogharimu jumla ya Shilingi Bilioni 22.9, unatarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo na biashara katika Manispaa ya Songea kwa kuongeza thamani ya mazao, kukuza uchumi wa ndani, na kutoa ajira kwa wananchi wa maeneo husika.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mkurugenzi Muhoja alimtaka Mhandisi anayesimamia mradi huo kuhakikisha anafanya kazi kwa uweledi wa hali ya juu, uwajibikaji, na kuzingatia muda uliopangwa. Pia alisisitiza umuhimu wa kuwa na mipango madhubuti ya kazi hususan katika kuzingatia msimu wa mvua unaokuja, ili mradi usikwame wala kucheleweshwa.
“Ninamtaka Mhandisi ahakikishe kazi hii inafanyika kwa viwango vya juu, kwa uadilifu, na kwa kuzingatia muda. Tunahitaji kuona tija kwa wananchi wetu, na hatutakuwa tayari kuona ucheleweshaji wowote unaotokana na kutozingatia hali ya hewa au maandalizi duni,” alisema Muhoja.
Kwa upande wake, mhandisi wa kampuni hiyo aliahidi kutekeleza mradi huo kwa kuzingatia viwango vya kimataifa na kuhakikisha unakamilika kwa wakati kama ilivyopangwa.
Makabidhiano hayo yamepokelewa kwa matumaini makubwa na wananchi, ambapo wengi wameeleza kuwa mradi huo utasaidia kuboresha miundombinu ya masoko na kuimarisha mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo kwa wakulima wa maeneo hayo.
Ujenzi unatarajiwa kuanza rasmi katika kipindi kifupi kijacho mara baada ya maandalizi ya awali kukamilika
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa