Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea, Wakili Muhoja, leo tarehe 22 Julai 2025 amekutana na watumishi wa Manispaa hiyo katika kikao cha ndani chenye lengo la kusikiliza na kupokea changamoto mbalimbali zinazowakabili watumishi hao.
Kikao hicho kimefanyika kwa mujibu wa utaratibu wake wa kawaida wa kukutana na watumishi kila baada ya miezi mitatu ili kujenga mawasiliano ya moja kwa moja, kuimarisha uwazi, na kuendeleza mshikamano katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku.



Katika hotuba yake, Wakili Muhoja amewataka watumishi wote kuendelea kudumisha nidhamu na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma, kuwajibika ipasavyo, pamoja na kuheshimu haki na stahiki za watumishi kama vile likizo, mafao ya likizo, posho, na vitendea kazi.
"Ni wajibu wa kila mtumishi kuhakikisha anatimiza majukumu yake kwa uadilifu na kutoa huduma bora kwa wananchi. Haki za watumishi ni suala lisiloepukika, lakini pia ni lazima tuheshimu wajibu wetu," alisisitiza Mkurugenzi.
Akiwaasa watumishi kuhusu kuanza kwa mwaka mpya wa fedha, Mkurugenzi huyo amezitaka idara na vitengo vyote kuandaa kwa wakati mpango wa manunuzi ya vitendea kazi ili kuondoa changamoto zinazoathiri utekelezaji wa majukumu yao.

“Ni muhimu kila idara kupanga mapema manunuzi ya vifaa vinavyohitajika ili kuepusha vikwazo katika utoaji wa huduma. Tujitume na tusimamie utekelezaji wa majukumu yetu kwa tija na ufanisi,” ameongeza.
Amesisitiza umuhimu wa watumishi kushirikiana kwa karibu na kutoa huduma bora kwa wananchi kama sehemu ya kuimarisha imani ya umma kwa Serikali yao.
Amina Pilly
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Manispaa ya Songea.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa