MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Nyasa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo kuhakikisha kuwa wanasimamia mradi wa ujenzi wa hospitali ya Wilaya hiyo na kukamilisha majengo yote saba kabla ya Juni 30 mwaka huu.
Mndeme amtoa agizo hilo baada ya kufanya ziara ya siku moja ya kukagua miradi inayotekelezwa katika Wilaya hiyo ukiwemo mradi wa hospitali ya wilaya,ofisi na nyumba ya Mkuu wa Wilaya ya Nyasa.
Amesema serikali inayoongozwa na Rais Dkt John Magufuli imetoa shilingi bilioni 1.5 za kutekeleza mradi wa hospitali hiyo hivyo hakuna sababu ya kuchelewa kutekeleza mradi huo ndani ya mkataba.
Taarifa ya ujenzi wa hospitali hiyo iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa Jimson Mhagama inaonesha kuwa jumla ya shilingi bilioni 1.5 zinajenga majengo saba ambayo ni jengo la utawala,wagonjwa,stoo ya dawa,maabara,vipimo vya mionzi,jengo la kufulia nguo na jengo la wazazi.
“Mikakati iliyopo ni kufanyakazi ya ujenzi wa hospitali usiku na mchana ili majengo yote yaweze kukamilika kufikia Juni 30,2019’’,anasisitiza Mhagama.
Wilaya ya Nyasa ina vituo 35 vya kutolea huduma ya Afya,vituo vya afya vitano,zahanati 28 na hospitali mbili ambazo zinamilikiwa na mashirika ya dini.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Awamu ya Tano ambayo inaongozwa na Rais Dkt.John Magufuli imelenga kukamilisha ujenzi wa hospitali katika Wilaya 67 za Tanzania ikiwemo Wilaya ya Nyasa ili kuboresha huduma za Afya kwa wananchi.
Imeandikwa na Albano Midelo
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa