Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmes Abbas Ahmed, amewapongeza vijana wa mkoa huo kwa muitikio mkubwa waliouonesha katika kushiriki kongamano la vijana, na kuwataka kuchangamkia fursa mbalimbali za kiuchumi na kibiashara.
Akizungumza katika kongamano hilo lililofanyika tarehe 5 Desemba 2025 katika ukumbi wa Songea Club, Mkuu wa Mkoa alisema lengo la mkutano huo ni kuhamasisha vijana kuwajibika katika shughuli za maendeleo ya jamii, huku kaulimbiu ikiwasisitiza vijana kujenga na kuilinda Ruvuma.
Alisisitiza umuhimu wa vijana kuwa mabalozi wa amani na kuonyesha matendo chanya kwenye jamii, akibainisha kuwa fursa nyingi za kiuchumi ni “dhahabu” endapo zitatumiwa ipasavyo. Aliongeza kuwa vijana wana nafasi kubwa katika kuchangia maendeleo ya taifa, hususan katika kuongeza thamani ya mazao kupitia kilimo cha kisasa.
Aidha, alieleza kuwa serikali inaendelea kuboresha mazingira rafiki kwa vijana, ikiwemo upatikanaji wa mitaji, mafunzo ya ujasiriamali na miundombinu ya kiuchumi. Aliwahimiza pia kutumia mitandao ya kijamii kwa malengo chanya kama vile kujifunza na kujiendeleza.
Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea, Mhe. Abraham Mbunda, aliwataka vijana kuwa mfano wa kuigwa katika nidhamu, amani na uadilifu, akisema kuwa wao ndio nguzo kuu ya jamii.
Naye mwakilishi wa vijana, Bw. Angelus Mvanda, aliishukuru serikali ya mkoa kwa kuwapatia vijana fursa za maendeleo na kuhimiza umoja miongoni mwao. Kwa niaba ya vijana, aliahidi kuongeza ushiriki wao katika sekta za kilimo, biashara, uchumi na viwanda.
Kongamano hilo lilihudhuriwa na viongozi wa ngazi ya mkoa, wawakilishi wa vyama vya siasa, vijana kutoka maeneo mbalimbali, pamoja na wadau wa maendeleo.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa