Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, ameweka jiwe la msingi katika ujenzi wa Duka la Dawa linalojengwa katika Kituo cha Afya Mjimwema, Manispaa ya Songea, akiwa katika ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Akizungumza mara baada ya kuweka jiwe hilo la msingi, Kanali Ahmed ameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Songea kwa kuibua na kutekeleza mradi huo muhimu unaolenga kusogeza huduma za afya karibu zaidi na wananchi.
“Kunapokuwa na huduma zinazofikiriwa kutolewa kwa wananchi, ni lazima zikamilike kwa wakati ili waweze kunufaika na huduma hizo,” alisema Kanali Ahmed.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kukamilika kwa wakati kwa mradi huo, hasa ikizingatiwa kuwa unatarajiwa kuzinduliwa rasmi kupitia Mbio za Mwenge wa Uhuru.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa alitembelea pia mradi wa ujenzi wa Maegesho ya Malori katika Kata ya Lilambo na kueleza kuridhishwa na maendeleo ya utekelezaji wake. Alitoa wito kwa viongozi wa maeneo husika kuendelea kushirikiana na Serikali ili miradi hiyo ianze kuleta mapato yatakayowezesha maendeleo kwa maeneo mengine.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Mjimwema, Bi. Alice Kitindi, alisema kuwa mradi huo ulianzishwa na Mganga Mkuu wa Manispaa ya Songea tarehe 6 Januari 2025 na unatarajiwa kukamilika tarehe 6 Mei 2025, ukiwa na unalenga kupunguza umbali wa wananchi kufuata huduma za dawa.
Bi. Kitindi alieleza kuwa hadi sasa ujenzi huo umefikia asilimia 99 ya utekelezaji, ambapo umegharimu shilingi 72,389,742/= licha ya makadirio ya awali kuwa shilingi 68,674,652.50.
Naye Diwani wa Kata ya Mjimwema, Mhe. Sylivesta Mhagama, alibainisha kuwa mradi huo unatekelezwa kwa kutumia fedha za mapato ya ndani, na ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha kuwa changamoto ya upatikanaji wa huduma ya dawa kwa wananchi wa kata hiyo inatatuliwa kwa haraka na ufanisi.
Na;
AMINA PILLY
KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa