MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amezindua kampeni ya watumishi wa umma kujiunga na mtandao wa TTCL kwenye ukumbi wa sekondari ya Songea Girls mjini Songea.
Akizungumza kabla ya uzinduzi huo,Mndeme alisema ni muhimu kwa watumishi wa umma kutumia mtandao wa TTCL ili waweze kujiimarisha kwa kupanua huduma na kuzalisha faida.
Amesema TTCL imekuwa inatoa gawio kwa serikali na kwamba Rais Dkt.John Magufuli huitumia faida inayotolewa na TTCL katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Tanzania.
Amesema serikali ya Awamu ya Tano imekusudia kuliimarisha Shirika la TTCL na kwamba shirika hilo ni nembo pekee ya kumkumbuka baba wa Taifa ndiyo maana linatakiwa kuimarishwa kwa Taasisi za serikali kwa kutumia huduma zake katika shughuli za mawasiliano.
“Serikali hii inatambua mchango wa mawasiliano na Shirika la Mawasiliano la Tanzania katika kuleta maendeleo yanayofikia na uchumi wa viwanda,mawasiliano ni muhimu sana katika kukuza uchumi kupitia simu za mezani,mkononi,intaneti na data’’,alisisitiza.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma ameagiza Taasisi zote za serikali zilizopo katika Mkoa wa Ruvuma ambazo hazijaanza kutumia laini za mtandao wa TTCL kwa ajili ya mawasiliano zianze mara moja.
Amewaagiza viongozi wa serikali katika Mkoa ,wanaolipwa vocha za mawasiliano na serikali,watumie laini za TTCL na kwamba lengo la serikali sio kuwazuia watu kutumia mitandao mingine bali ni kuimarisha TTCL ambacho ndiyo chombo cha mawasiliano cha serikali.
“Wakati sasa umefika sasa watumishi wa umma kuunga mkono juhudi za serikali za kuimarisha mtandao wa TTCL kwa manufaa ya uchumi wa nchi yetu’’,alisisitiza Mndeme.
Meneja wa TTCL Mkoa wa Ruvuma Zabron Magabula amesema idadi ya watumiaji wa mtandao wa TTCL ni ndogo ambapo kutokana na mfumo wa usajili wa watumishi wa umma kuna jumla ya watumishi 102 katika Mkoa wa Ruvuma.
Amesema kati ya watumishi hao Manispaa ya Songea watumishi 38,Songea vijijini 26,Tnuduru 24,Mbinga 12 na Nyasa sita na kwamba idadi hiyo ni ndogo ukilinganisha na idadi ya watumishi wa umma waliopo mkoani Ruvuma.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Serikalini
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa