BENKI ya NMB imedhamiria katika kutoa huduma za kibenki za kidigitali kwa watanzania wote ili kuweza kufanya miamala na malipo mbalimbali kwa ufanisi na kasi zaidi.
Akizungumza katika kongamano la walimu na NMB Wilayani ya Songea mkoani Ruvuma lililofanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea,Afisa Mwandamizi wa Amana za wateja binafsi kutoka NMB Makao makuu, Isaack Mgwassa anasema njia hiyo ni bora zaidi na inaendana na kasi ya ukuaji wa teknolojia ambayo itasaidia kuleta mwamko mkubwa kwa watanzania.
“NMB imeona ni muhimu kukutana na wadau wake wakubwa katika huduma za kibenki hivyo imetenga siku maalum ya kuzungumza na wateja na kuwapa maendeleo ya benki yao na huduma mbalimbali zinazotolewa ili kuwapa uelewa zaidi’’,anasema Mgwassa.
Anasema kupitia kongamano la walimu watapata mrejesho na mawazo mbalimbali kuhusiana na huduma za NMB ambayo yatasaidia kufanya maboresho.
Anasema NMB inaamini kupitia waratibu Elimu Kata na walimu wakuu katika shule za msingi na sekondari katika Wilaya ya Songea,watasaidia kupeleka elimu watakayoipata kwa walimu wenzao na jamii yote kwa ujumla kuhusiana na huduma bora za NMB zinazomgusa kila Mtanzania.
Hata hivyo anasema utafiti umebaini kuwa licha ya watanzania kufikia zaidi ya milioni 50,ni asilimia chini ya 40 tu ndiyo wenye akaunti benki na kwamba zaidi ya asilimia 60 ya watanzania wanamiliki simu za mkononi na wana uwezo wa kufanya malipo na miamala kupitia simu za mkononi.
Kulingana na Meneja Mwandamizi huyo,NMB katika nchi nzima ina wateja zaidi ya milioni 3.2 kati yao zaidi ya wateja milioni 2.5 wanatumia simu kufanya miamala,kuangalia salio,kufanya malipo mbalimbali,kulipia umeme na kodi mbalimbali.
“Tumedhamiria kuona NMB inakuwa Benki ya kwanza Tanzania kuanzisha mfumo wa kutotumia fedha unapokuwa kwenye shughuli zako bali kutumia kadi na simu za mikononi kufanya manunuzi na matumizi mengine ya fedha zako zilizopo Benki’’,anasisitiza Mgwassa.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme ambaye aliwakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro akizungumza kabla ya kufungua kongamano hilo ametoa rai kwa NMB kuendelea kutoa elimu ya huduma za kibenki kutokana na takwimu kuonesha ni chini ya asilimia 40 ya watanzania ndiyo wenye akaunti benki.
“Kuna kila sababu ya vyombo vya fedha kuwa na program maalum ya kutoa elimu hasa katika maeneo ya vijijini ili waweze kupata elimu sahihi na kufaidika na huduma za kifedha zinazotolewa na benki hapa Tanzania’’,anasema Mndeme.
Mndeme ameipongeza NMB kwa kutoa mikopo mingi kwa wafanyakazi wa serikali kuu na serikali za mitaa na kwamba asilimia kubwa ya walimu hapa nchini wamefaidika na mikopo ya benki hiyo.
Takwimu za Benki ya NMB zinaonesha kuwa hadi sasa imetoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni mbili ikiwa ni mikopo kwa wafanyakazi kiwango ambacho amesema ni kukubwa kuwahi kutolewa na Taasisi za kifedha nchini.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa ametoa rai kwa NMB kuendelea kuandaa program nyingi kwa watumishi wote wa serikali ili kuwapatia fursa ya kujua huduma zinazotolewa na Benki na kuendelea kubuni bidhaa mbalimbali za kibenki ambazo mtumishi wa kawaida anaweza kumudu.
“Endeleeni kupanua wigo wa mikopo,na mikopo yenu iwe na riba nafuu,pia endeleeni kuboresha huduma kwa wateja ili idadi yao iweze kuongezeka na kupata fursa nyingi za kukopo kwa masharti nafuu na kuongeza tija kwenye maeneo yao ya kazi’’,anasisitiza Mndeme.
Daniel Zake ni Meneja wa NMB tawi la Songea akitoa shukrani za NMB kwa mgeni rasmi, ameeleza kuwa Benki hiyo ina matawi 223 nchi nzima,ATM zaidi ya 800 na wakala zaidi ya 7000 ambapo anasema Benki hiyo ni sikivu ipo tayari kusikiliza changamoto za wateja kama walimu na kuzitafutia ufumbuzi.
Zake amemthibitishia Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kuwa suala la riba litafanyiwa kazi na uongozi wa NMB na kwamba kwa kanuni za benki kuna vikao mahususi kwa ajili ya kupitisha vitu vya namna hiyo.
Naye Mwakilishi wa Afisa Elimu Mkoa wa Ruvuma Musa Musa anasema Benki ya NMB ni nguzo muhimu kwa watumishi wa umma wakiwemo walimu kwa sababu imekuwa inatoa mikopo mbalimbali kwa riba nafuu hali ambayo imesababisha walimu wengi kujenga nyumba,kusoma na kusomesha watoto wao katika ngazi mbalimbali za elimu.
Ametoa rai kwa walimu na watanzania wengine kwa ujumla kuendelea kutumia huduma zinazotolewa na Benki ya NMB kutokana na huduma zake kuwa bora,usalama na uhakika.
Jane Nyandindi ni Mkuu wa shule ya sekondari ya Lukala katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea ambaye ni mmoja wa wateja wa Benki ya NMB, anasema amefurahishwa na kongamano la walimu na NMB ambapo kupitia hafla hiyo, wamepata mwanga wa kutosha kuhusiana na huduma mbalimbali za NMB.
Nyandindi anasema amekuwa mteja wa NMB tangu mwaka 1999 na kwamba tangu wakati huo amenufaida na mikopo ya benki kwa watumishi ambayo imemsaidia kupata maendeleo mbalimbali.
Vitus Ngoma ni Mkuu wa shule ya msingi Mashujaa katika Manispaa ya Songea anasema kongamano la NMB limemwezesha kutambua kwa kina huduma mbalimbali za Benki ya NMB.
Anasema tangu amekuwa mteja wa NMB ananufaika na huduma mbalimbali zikiwemo kupokelea mshahara,kupata mikopo na kwamba huduma karibu zote zinazotolewa ndani ya benki hiyo zinawaridhisha wateja wake.
Hata hivyo ametoa rai kwa Benki hiyo kuboresha kipengele cha mikopo ili kupunguza riba kwa wateja ambacho kinaleta changamoto kwa watumishi .
Kongamano hilo limewashirikisha walimu wakuu,waratibu elimu Kata na watendaji waandamizi wa elimu kutoka Wilaya Songea zaidi ya 230
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa