Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, amewataka wataalamu wa sekta mbalimbali kuwa na utamaduni wa kuishirikisha jamii pamoja na wadau wakati wa kufanya maamuzi yanayohusu maendeleo ya wananchi.
Akizungumza wakati wa ziara yake tarehe 14 Aprili 2025 katika Manispaa ya Songea, Kanali Ahmed alisisitiza umuhimu wa kuwepo kwa vikao vya ushirikishwaji kabla ya kutoa maagizo au kufanya maamuzi muhimu.
"Mnapotaka kutoa maagizo, hakikisheni mnaweka vikao vya kushirikisha jamii juu ya jambo husika, hii itasaidia kutoa elimu kuhusu fursa zilizopo na kuwapa wananchi taarifa sahihi kuhusu maendeleo yanayofanywa na Serikali yao," alisema.
Katika ziara hiyo, Mkuu huyo wa Mkoa alitembelea maeneo ya Stendi ya Ruhuwiko na Mfaranyaki ambapo alisikiliza changamoto mbalimbali kutoka kwa wafanyabiashara na wananchi ambapo alibainisha kuwa Serikali inafanya jitihada kubwa katika kuboresha huduma kwa wananchi, ikiwemo na kutekelezwa kwa miradi mikubwa ya maendeleo kama ikiwemo na Mradi mkubwa wa maji wenye thamani ya Shilingi Bilioni 145, Ujenzi wa barabara ya mchepuko (Bypass) ya Songea pamoja na Ujenzi wa masoko 2 ya Manzese
Kanali Ahmed alisema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliahidi kutatua tatizo la msongamano wa magari makubwa (maroli) katika mji wa Songea, ambapo alithibitisha kuwa fedha za ujenzi wa barabara ya mchepuko zimeshapokelewa na maandalizi ya kuanza ujenzi huo yako tayari.
Akizungumzia suala la usalama wa wasafirishaji wa bodaboda na bajaji, alieleza umuhimu wa kuwa na sare maalum kwa ajili ya utambulisho wa madereva hao. "Ni muhimu madereva wa bodaboda na bajaji wawe na sare ili waweze kutambulika kirahisi hasa wanapopata matatizo au kutambulika wanapofanya kazi na Hii pia itasaidia kupunguza athari kutoka kwa maroli na mabasi," alisema.
Katika hatua ya awali, tayari sare 300 za kuakisi mwanga (reflector jackets) zimepatikana kwa ajili ya kugawiwa kwa madereva hao.
Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea, Michael Mbano, alieleza kuwa Serikali imetekeleza agizo la Rais kwa kutenga eneo maalumu la Wamachinga katika eneo la Majengo, Hata hivyo, bado baadhi yao hawajaanza kulitumia.
"Tunatoa wito kwa wafanyabiashara ambao hawajapata maeneo wafike ofisini kwa Mstahiki Meya ili waweze kupewa nafasi ya kufanyia biashara zao kihalali," alisema Mbano.
Aidha, alitoa wito kwa wananchi kuwa wavumilivu wakati Serikali ikijiandaa kuanza rasmi ujenzi wa soko la Manzese, ambapo taratibu zote muhimu tayari zimekamilika na utekelezaji wake unatarajiwa kuanza hivi karibuni.
Kwa upande wa wafanyabiashara hao waliishukuru viongozi hao kwa kuwatembelea na kubaini chanmgamoto zinazowakabili ambapo Serikali imeahidi kuzitatua.
IMEANDALIWA NA
AMINA PILLY
KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa