Songea Mjini, tarehe 12 Septemba 2024 Mkuu wa Wilaya ya Songea, Kapenjama Ndile, amewapongeza wananchi wa Songea Mjini kwa kujitokeza kwa wingi na kupeleka mbwa wao katika maadhimisho ya uchanjaji wa chanjo ya kichaa cha mbwa. Maadhimisho hayo yalifanyika katika viwanja vya shule ya sekondari Matarawe, Songea Mjini.
Ndile amesisitiza umuhimu wa chanjo hiyo katika kuzuia hatari ya kichaa cha mbwa na kuwasihi wale ambao hawakupata nafasi ya kuchanja mbwa wao kujitahidi kuhakikisha mchakato huo unakamilika. "Chanjo ni muhimu kwa usalama wa jamii, hivyo ni lazima kuhakikisha kuwa mbwa wote wanapewa chanjo ili kupunguza hatari ya ugonjwa huu," alisema Ndile.
Aidha, Mkuu wa Wilaya amewataka wananchi kutunza mbwa wao kwa njia ya kisasa, ikiwa ni pamoja na kuwajengea mabanda ya kisasa, kuwafungia wakati wa mchana, na kuwaweka katika mazingira bora kwa kuwapa chakula chakutosha. "Hii itasaidia kuboresha hali ya mbwa na kuhakikisha wanakuwa na afya njema," aliongeza Ndile.
Kwa upande wake, Daktari wa Mifugo, Seria Masole Shonyera, ameipongeza serikali kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea katika uratibu wa zoezi hili la chanjo. Shonyera alisema kuwa chanjo ya bure iliyoandaliwa imewezesha kufanikisha uzinduzi wa maadhimisho haya na kutoa msaada mkubwa kwa jamii.
Maadhimisho haya ya kichaa cha mbwa duniani yanafanyika kila mwaka tarehe 28/09, lakini kwa wilaya ya Songea Mjini, yamefanyika mapema mwaka huu kutokana na shughuli nyingine zinazotarajiwa kufanyika katika tarehe hiyo.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa