Katika juhudi za kuboresha sekta ya pembejeo na kilimo, Mkuu wa Wilaya ya Songea, Wilaman Kapenjama Ndile, leo ameongoza mkutano wa muhimu uliofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Songea ambapo Mkutano huu uliwaleta pamoja wafanyabiashara wa pembejeo, wakulima, na maafisa wa serikali kwa ajili ya kujadili changamoto na mikakati ya kuimarisha sekta hiyo.
Katika hotuba yake, Mheshimiwa Ndile alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa karibu kati ya serikali na wafanyabiashara katika kuhakikisha upatikanaji wa pembejeo bora kwa wakulima pia Alieleza kuwa serikali imejitolea kuboresha mifumo ya usambazaji na udhibiti wa ubora wa pembejeo ili kuondoa changamoto za ucheleweshaji na ubora wa bidhaa zinazopatikana sokoni.
"Ubora wa pembejeo ni suala la msingi ambalo linahitaji umakini wa hali ya juu, pia Tunahitaji kuhakikisha kwamba pembejeo zinazouzwa zinakidhi viwango vya ubora vilivyowekwa na mamlaka husika," alisema Mheshimiwa Ndile.
Aliongeza kuwa serikali itatekeleza mfumo madhubuti wa ukaguzi wa ubora wa pembejeo na kuimarisha udhibiti wa bei ili kuhakikisha bei za pembejeo zinakuwa rafiki kwa wakulima.
Wafanyabiashara walipokea mwito wa Mheshimiwa Ndile kwa mikono miwili na walionesha kujitolea katika kuhakikisha kuwa huduma zao zinakidhi viwango vya ubora na bei zinazokubalika pia Walisema watashirikiana na serikali katika kuboresha mifumo ya usambazaji na kutoa mapendekezo kuhusu changamoto wanazokumbana nazo.
Mkutano huu pia uliwashirikisha wafanyabiashara katika kujadili masuala ya bei, ubora wa pembejeo, na ushirikiano wa mawasiliano kati ya pande zote ambapo Viongozi wa serikali walipokea maoni na mapendekezo kutoka kwa wafanyabiashara na wakulima kwa lengo la kutatua changamoto zinazojitokeza.
Mkuu wa Wilaya alimalizia kwa kutoa shukrani kwa washiriki wote na kuwatia moyo kuendelea na juhudi zao za kuboresha sekta ya pembejeo pia alisisitiza kwamba kwa ushirikiano wa karibu, changamoto zitakazokabiliwa zinaweza kutatuliwa kwa ufanisi na maendeleo ya sekta hiyo yataimarika.
AMINA PILLY
KITENGO CHA MAWASILIANO