UKARABATI wa mradi wa bustani ya Manispaa ya Songea umekamilika na unatarajia kuanza kufanyakazi wakati wowote mwaka huu,ambapo Mkandarasi tayari amekabidhi mradi huo kwa Manispaa.
Mhandisi wa Idara ya ujenzi wa Manispaa ya Songea Mhandisi Caroline Bernad amesema mradi ulikamilika tangu Desemba 2017 ambapo Mkandarasi alipewa matazamio ya miezi sita ya mradi huo ambayo yaliishia Aprili 2018.
Amezitaja kazi zilizosalia kuwa ni kuendelea kuotesha nyasi,kufunga mfumo wa maji taka ambayo inafanywa na Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (SOUWASA) na kuweka nishati ya Umeme kazi ambazo zinatarajia kukamilika mwezi huu.
Amesema Kitengo cha manunuzi kimeshatangaza zabuni ya uendeshaji wa bustani ya manispaa.Kazi zilizofanyika na kukamilika katika bustani hiyo ni ujenzi wa mgawaha,choo,uzio,michezo ya watoto(bembea),sehemu za kupumzikia na maegesho ya magari kuzunguka bustani.
Maeneo mengine ni utengenezaji wa viunga,miti na nyasi,ujenzi wa maeneo ya kupaki magari,usambazaji wa mabomba ya maji katika eneo la bustani,ujenzi wa mnara,ukarabati wa mnara,kufunga bembea na kufunga taa za 12 za sola.
“Mradi hadi sasa umekamilika kabisa na umekabidhiwa tangu Mei 15,2018 na upo tayari kwa ajili ya kutumika,hivyo wakati tunasubiri mchakato wa manunuzi kukamilika kwa ajili ya kumpata mtu wa kuendesha,imeshauriwa Halmashauri kuweka mlinzi katika eneo la bustani’’,anasisitiza Mhandisi.
Mradi huo umefadhiliwa na Benki ya Dunia kwa gharama ya shilingi milioni 399.Hata hivyo hadi sasa Mkandarasi ameshalipwa zaidi ya milioni 361.
Wawakilishi wa Benki ya Dunia wameukagua mradi huo na kuridhishwa na kiwango cha ujenzi wa bustani hiyo ambayo inavutia wengi kwa kuwa imebadilisha muonekano wa mji wa Songea.
Imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Agosti Mosi,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa