Na,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
16.11.2021
Wilaya ya Songea kuanza utekelezaji wa mradi wa REA kwa awamu ya tatu mzunguko wa pili ili kufikia maeneo ambayo bado hayajapata huduma ya umeme.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Kamando Mgema wakati akiongoza kikao kazi cha kamati ya ushauri ya Wilaya ya Songea hapo jana tarehe 15 Novemba 2021, kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Songea na kuhudhuriwa na wajumbe mbalimbali wa kamati hiyo wakiwemo wakurugenzi wa Halmashauri kutoka Manispaa ya Songea, Madaba na Wilaya ya Songea.
Mgema alisema kuwa Serikali imejipanga kusimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ndani ya Wilaya ya Songea kwa kuhakikisha wanapeleka huduma muhimu kwa wananchi katika maeneo mbalimbali hasa maeneo yaliyopo vijijini ikiwemo na miundombinu ya umeme, maji, elimu na afya.
Aliongeza kuwa wataalamu wanatakiwa kutimiza wajibu kwa kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo yao kwa wakati ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya elimu na maji inayoendelea kutekelezwa kwenye maeneo mbalimbali ndani ya Wilaya ya Songea.
Ametoa rai kwa wananchi kuacha tabia ya kuhujumu miundombinu ya umeme ambapo limeibuka wimbi kubwa la wizi wa kebo kwenye transifoma na kusababisha hasara kwa Serikali na amelitaka jeshi la polisi kuhakikisha wanachukua hatua kali kwa yeyote atakayebainika anahusika na matukio hayo.’Alisisitiza’
Amewataka viongozi na wataalamu wa mazingira kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na namna ya kutunza mazingira ikiwemo na utunzaji wa vyanzo vya maji pamoja na misitu katika maeneo yao ili kuthibiti mabadiliko ya tabia ya nchi yaliyosababisha ongezeko kubwa la joto katika maeneo mbalimbali nchini.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakurugenzi wa Halmashauri zote 3 zilizopo ndani ya Wilaya ya Songea wameahidi kusimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao pamoja na zoezi zima la utoaji wa mikopo kwa vijana, wanawake na watu wenye mahitaji maalumu kwa kuhakikisha mikopo hiyo inaleta tija na maendeleo kwa vikundi hivyo pamoja na kurejeshwa kwa wakati.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi (CCM) Nelly Duwe ametoa pongezi kwa viongozi wa Wilaya ya Songea kwa kukubali kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kama ilivyoainishwa katika Ilani ya chama cha mapinduzi na amewataka kuwashirikisha changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika kipindi cha utekelezaji wa miradi ili waweze kuzitatua kwa pamoja.
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa