Mstahiki Meya Manispaa ya Songea Michael Mbano amewataka Waheshimiwa Madiwani na Wataalamu wote kuendelea kufanya uhamasishaji katika kata zao na kuendelea kuwahimiza wananchi kujitokeza kuhesabiwa Sensa ya watu na makazi ambayo leo hii ni siku ya nne toka zoezi hilo lianze kufanyika.
Rai hiyo imetolewa leo tarehe 26 Agosti 2022 katika Mkutano wa Baraza la Madiwani uliofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Songea na kuhudhuriwa na Madiwani, Wananchi mbalimbali, Wataalamu na viongozi wa vyama vya siasa ambacho ni kikao cha kuhitimisha taarifa kwa mwaka wa fedha 2021 hadi 2022.
Mbano akihitimisha baraza hilo huku akitoa taarifa za kuwakaribisha wananchi wote katika Mkutano wa Mwaka wa Baraza la Madiwani ambao unatarajia kufanyika hapo kesho tarehe 27 Agosti 2022 katika ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea.
Akihutubia Mkutano wa Baraza la Madiwani Waziri wa Katiba na Sheria DKT. Damas Ndumbaro(MB) alisema “ Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha Tozo na Kodi ambayo hulipwa na wananchi kwa ajili ya Maendeleo ya Taifa letu na hatimaye hurudishwa asilimia kwenye Halmashauri mbalimbali ambazo husaidia jamii kwa maendeleo ya Nchi yetu” Alisisitiza.
Alisema Kodi inasaidia Serikali kupata Maendeleo ambapo kwa Manispaa ya Songea imesaidia kujenga miradi mbalimbali ya maendeleo ambapo katika kipindi cha mwaka 2021/2022 Manispaa ya Songea imewezesha kujenga vituo vya afya vitano 5, ujenzi wa Hospitali ya Manispaa ya ambayo inajengwa katika kata ya Tanga, Ujenzi wa Masoko mawili ya kisasa ya Manzese, pamoja na ujenzi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Ruvuma.
Dkt. Ndumbaro (MB) amebainisha kuwa ataendelea kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wa Jimbo la Songea Mjini kwa lengo la kusimamia na kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Hamisi Abdallah Ally amewataka wataalamu kusimamia vizuri zoezi la usajili wa wakulima wanaohitaji pembejeo na kuondoa malalamiko mbalimbali ambayo yanaweza kujitokeza.
Mhe. Hamisi amesema Maafisa kilimo wanatakiwa kufanya kazi kwa weredi na kuhakikisha wananchi wanapata pembejeo ya Ruzuku kwa wakati na kwakuwa wamepewa vyombo vya usafiri watatakiwa kuwafikia wakulima kwa wakati na kutatua changamoto zao.
Waheshimiwa Madiwani kwa umoja wao wamepokea maagizo yaliyotolewa kwenye kikao hicho na wameahidi kutoa ushirkiano kwenye kata zao.
Imeandaliwa na;
AMINA PILLY
AFISA HABARI MANISPAA YA SONGEA.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa