Manispaa ya Songea mwaka huu imedhamiria kuibuka kidedea katika mashindano ya mapokezi ya Mwenge wa Uhuru baada ya kuweka maandalizi mazuri.
Mwenge wa Uhuru Manispaa ya Songea unatarajia kupokelewa kesho Juni 7,2018,katika shule ya Msingi Mang’ua Kata ya Lilambo na unatarajiwa kukabidhiwa katika Halmashauri ya Madaba Juni 8 mwaka huu.
Kwa mujibu wa Mratibu wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Manispaa ya Songea Faraja Yonasi,Mwenge wa Uhuru ukiwa katika Manispaa ya Songea unatarajia kutembelea,kuweka mawe ya Msingi na kuzindua miradi mbalimbali.
Kulingana na Ratiba ya Mwenge jumla ya miradi tisa yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 945 inatarajiwa kupitiwa na Mwenge wa Uhuru. Miongoni mwa miradi hiyo ni mradi wa zahanati binafsi ya St Benjamin iliyopo katika Kata ya Msamala. Mwenge wa Uhuru unatarajia kufanya uzinduzi wa zahanati hiyo.
Miradi mingine ambayo inatarajiwa kupitiwa na Mwenge wa Uhuru ni mradi wa mabwawa ya kisasa ya ufugaji samaki na utalii wa ndani Luhira kata ya Msamala, mradi wa maji Mitendewawa kata ya Mshangano, mradi wa madarasa matatu shule ya msingi Kibulang,oma kata ya Lizaboni, mradi wa kopa ng,ombe lipa ng'ombe kata ya Lilambo, mradi wa kiwanda cha kukoboa mpunga katika Kata ya misufini na mradi wa ofisi ya Kata ya Mjimwema.
Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Mgema ameendelea kuwasisitizia wakuu wa Idara,Vitengo,madiwani na maafisa watendaji kushirikiana kujenga hamasa ili kuhakikisha kuwa Manispaa hiyo mwaka huu inashika nafasi za juu kwenye mashindano ya Mbio za Mwenge wa Uhuru.
“Haya ni mashindano,vimewekwa vigezo ili kushinda,sitaki mchezo katika suala la Mwenge,atakayeshindwa kuwajibika,tutachukuliana hatua,Mwenge ni sherehe ili kufanikiwa kila mmoja ni lazima atekeleze majukumu yake’’,anasisitiza Mkuu wa Wilaya.
Ujumbe wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2018;
-Elimu ni Ufunguo wa maisha
-Wekeza sasa kwa maendeleo ya Taifa letu
-Mwananchi jitambue pima afya yako
-Kataa rushwa jenga Tanzania
-Shiriki kutokomeza malaria
-Tuwasikilize na kuwashauri watoto wasitumie dawa za kulevya
Taarifa imetolewa na
Albano Midelo
Afisa Habari na Mawasiliano,Manispaa ya Songea
Juni 6,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa