Ushirikishwaji na uwajibikaji wa viongozi kwa wananchi ni sehemu ya utawala bora kwa kiongozi, hivyo kila Mheshimiwa diwani katika Kata yake anatakiwa kuwashirikisha wadau wa maendeleo waliopo kwenye kata husika kwa ajili ya kusaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii.
Hayo yametamkwa na Naibu Meya Jeremia Milembe kwa niaba ya Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Michael Mbano katika kikao kazi ambacho kilihudhuriwa na Maafisa watendaji wa kata, Waheshimiwa Madiwani, pamoja na Wakuu wa Idara kilichofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Songea leo 16 februari 2021.
Jeremia alisema katika kikao kijacho atahitaji uwepo wa taarifa kutoka kila kata zikionesha aina ya changamoto na jinsi alivyoweza kuitatua ili waweze kubaini njia ya kusaidia kuzitatua changamoto zinazowakabili wananchi wa kata husika.
Kikao hicho hufanyika kabla ya kikao cha baraza la madiwani la Halmashauri ambacho hufanyika kwa lengo la kupokea taarifa mbalimbali za utekelezaji kutoka kila kata zinazojumuisha maendeleo ya elimu, miundombinu ya shule, Zahanati, maendeleo ya kilimo, mifugo, hali ya majanga, utawala, Uchumi, uimarishaji wa dhana ya uzalendo pamoja na kupokea changamoto mbalimbali kutoka kwenye kata na kufanyiwa ufumbuzi.
Jeremia amewataka wataalamu wa Manispaa kutoa ushirikiano kwa Madiwani ili kujenga ufanisi wa kiutendaji katika kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kwa lengo la kutoa huduma bora kwa jamii ya Songea.
Naye Afisa utumishi Mkuu Manispaa ya Songea Lewis Mnyambwa akitoa ufafanuzi kuhusu kikao cha utekelezaji ambapo alisema “ kanuni za kudumu za Halmashauri ya manispaa ya Songea Tangazo la Serikali Na 162 inasema taarifa za utekelezaji kutoka katika kata zitawasilishwa na Diwani wa kata husika au kama diwani hayupo, taarifa hiyo itawasilishwa na Diwani wa Viti maalum anayeishi katika Kata hiyo na kama Diwani Viti Maalum hayupo, Meya atamtaarifu mapema Diwani yeyote ili ajiandae kuwasilisha taarifa hiyo”.
Baraza hilo la Madiwani linatarajia kufanyika kesho 17.02.2021 katika ukumbi wa Manispaa ya Songea kuanzia muda wa saa tatu asubuhi.
IMEANDALIWA NA;
AMINA PILLY;
AFISA HABARI MANISPAA YA SONGEA.
16 .02.2021
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa