ENDAPO ulipewa Ilani ya siku 14 inayokutaka kulipa kodi ya ardhi na haijalipwa kodi hiyo utatakiwa kupelekwa kwenye baraza la ardhi na endapo hatalipa kodi hiyo atauziwa mali zake.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi DkT.Angeline S.L.Mabula akiwa ziarani Manispaa ya Songea iliyofanyika tarehe 24 februari 2021 katika ukumbi wa Manispaa ya Songea na kugawa hati 64 za umiliki wa ardhi.
DKT. Mabula alisema Lengo kuu la Serikali ni kumuongoza mwananchi wa kawaida katika kupata Hati yake ya umiliki wa ardhi ili awe anauwezo wa kutambua mipaka yake, kutatua migogoro, pamoja na kutumia kukopa fedha Benki sababu Hati ni pesa.
Alisema Ukusanyaji wa Maduhuli ya Serikali umekuwa chini sana ukilinganisha na hali halisi ya makusanyo ya maduhuli ambapo hadi hivi sasa makusanyo hayo yamefikia 16% kimkoa ambayo hadi kufikia june hatarajii kama watafikia 50%.
Alieleza kuwa sheria ipo wazi hata mwenye kiwanja ambacho hakina HATI anatakiwa kulipa kodi ya ardhi ambapo alisema kifungu cha 48 kifungu kidogo cha (1) G cha sheria namba (4) ya ardhi kinasema “unapopewa Ilani na ukakaanayo bila kulipa ndani ya miezi 6 ubatilishwaji wa umiliki unaweza kufanyika bila kupewa taarifa kwasababu tayari umekiuka sheria.”
Aliongeza kuwa kifungu cha 33 cha sheria namba (4) ya mwaka 1999 kwa marekebisho yaliyofanyika kwenye sheria ya fedha mwaka 2020 ambayo inasema “ yeyote mwenye kumiliki ardhi bila kujali ana HATI au hana HATI anatakiwa kuomba kumilikishwa ardhi na endapo hajaomba kumilikshwa atatakiwa kulipa kodi toka pale ambapo idhini ya ramani zake zilipitishwa.”
Ameagiza kutokana na wadaiwa sugu kuwa wengi na wengine kesi zao zipo kwenye mabaraza na wengine wana order na zimeshapelekwa kwenye baraza za ardhi ambapo amesema utekelezaji wake uanze sasa kwa kukamata mali zao na kuziuza ili kodi iweze kukusanywa kwa kiasi kikubwa.
Agizo hilo linatakiwa kutekelezwa mara moja na hadi kufikia aprili 31 utekelezaji wa sheria ambazo zilikuwa hazitekelezwi uwe umeanza kutekelezwa. Alisema DKT. Mabula.
Naye Kamishina wa ardhi Msaidizi Mkoa wa Ruvuma Ildefonce Ndemela alisema tangu kuanzishwa kwa ofisi ya Ardhi Mkoa, Ofisi imesimamia na kutekeleza kazi za upangaji, upimaji, umilikishaji, uthamini,usajili wa Hati na nyaraka mbalimbali, utatuzi wa migogoro ya Ardhi na ukusanyaji wa Maduhuli ya Serikali kama utawala wa Ardhi ambapo katika mwaka wa fedha 2019/2020 Mkoa wa Ruvuma ulipangiwa kukusanya fedha 1,076,957,356.22 sawa na 108%, ambapo kwa mwaka wa fedha 2020/2021 Mkoa wa Ruvuma umepangiwa lengo la kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 4.6.
IMEANDALIWA NA;
AMINA PILLY;
AFISA HABARI MANISPAA YA SONGEA.
25.02.2021
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa