Naibu waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia ametoa wiki moja kwa mtaalamu Elekezi kutoka Kampuni ya Archquants Service Limited kuhakikisha inawasilisha michoro ya kazi za nje ya Chuo cha ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi Namtumbo kilichoko Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma ili chuo hicho kiweze kukamilika na kuanza kazi.
Naibu Waziri Ole Nasha ametoa agizo hilo Mkoani Ruvuma wakati wa kukagua maendeleo ya ujenzi wa chuo hicho ambapo amesema ucheleweshwaji wa michoro hiyo unapelekea kuchelewesha ukamilishaji wa mradi huo.
Awali Mkandarasi anayejenga Chuo hicho CF Builders alimweleza Naibu Waziri kuwa mpaka sasa hajapokea michoro ya kazi za nje ya Chuo hicho jambo ambalo linasababisha kuchelewa kukamilisha mradi huo.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri Ole Nasha ameitaka Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi VETA kuhakikisha wanaanzisha kozi ya ufundi wa zana za kilimo (agro mechanics) katika Chuo cha Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi cha Songea VETA ili kuweza kupata vijana wengi watakaoweza kusoma kozi hiyo.
Alisema ukanda wa Nyanda za Juu Kusini unategemea sana kilimo na asilimia 60 ya chakula hutoka huko katika ukanda huo hivyo kuanzisha kozi hiyo itasaidia wananchi wengi kuweza kupata uelewa wa kile wanachokisoma katika kukifanyia kazi.
Alisema Nchi yetu iko kwenye jitihada za kufikia uchumi kati ambao unategemea msukumo wa viwanda na kama unazungumzia masuala ya uchumi wa viwanda ni lazima kuwa na mafundi hivyo Vyuo vya VETA vitasaidia kupata nguvu kazi watakaosaidia katika uchumi wa viwanda.
“Serikali inatilia mkazo Elimu ya ufundi na imejielekeza katika kuhakikisha inapanua fursa ya vijana wengi kupata hiyo na ndio maana unaona Serikali ya awamu ya tano imeamua kuweka Vyuo vya VETA katika kila Wilaya na Mkoa” Alisisitiza Naibu Waziri Ole Nasha
Ameipongeza VETA Songea kwa namna ambavyo wamebuni mbinu mbalimbali za kufikisha Elimu ya ufundi kwa wananchi wengi kwa kuwafikia katika maeneo yao na kuwataka kuendelea kushirikana na makampuni na mbalimbali wanapotoa mafunzo yao ili kujua uhitaji wa soko.
Naibu Waziri Ole Nasha yuko mkoani Ruvuma kwa siku mbili kukagua miradi ya Elimu inayotekelezwa na Wizara katika Wilaya za Namtumbo na Songea.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA.
01/10/2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa