NAIBU Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Josephat Kandege yupo mkoani Ruvuma katika ziara kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo,akiwa katika Manispaa ya Songea ameikagua miradi mbalimbali ikiwemo ya mradi wa barabara za lami katika Manispaa ya Songea.
Akiwa katika barabara ya Tumbani eneo la majengo Kandege amemwagiza Mkandarasi kuhakikisha kuwa barabara hiyo inawekwa lami nzito kabla ya mvua za masika hazijaanza Novemba mwaka huu kwa kuwa mvua zikiianza inakuwa ni kazi ngumu kuweka lami hivyo amewaagiza kuongeza kasi ili kusiwepo na kisingizio cha mvua.
Hata hivyo Mkandarasi huyo amemuahidi Waziri kuwa Kampuni yake imejipanga kuhakikisha kuwa kazi hiyo inakamilika ndani ya mkataba na kwamba katika barabara hiyo wamejipanga kuweka lami kabla ya mvua za masika kuanza kwa sababu iwapo mvua zitawakuta hawataweza kuweka lami.
Kampuni ya kimataifa ya China inayoitwa China Sichuan International Co-operation ndiyo imeshinda tuzo ya Zabuni ya kuendelea na ujenzi wa barabara za Manispaa ya Songea kwa kiwango cha lami nzito zenye urefu wa zaidi ya kilometa 10 kwa zaidi ya shilingi bilioni 10 na kwamba Kampuni hiyo pia itaweka taa za barabarani.Mkataba wa Barabara hizo ni wa miezi 18 kuanzia Machi 2018 hadi Septemba 30,2019.
Halmashauri ya Manispaa ya Songea ilivunja Mkataba wa ujenzi wa lami nzito yenye urefu wa kilometa 8.6 kati yake na Kampuni ya Lukolo yenye makao makuu yake Jijini Dar es salaam,baada ya Kampuni hiyo kukiuka masharti ya mkataba wa miaka miwili uliomalizika Juni 30 mwaka 2017.
Fedha za mradi huo ambazo ni zaidi ya shilingi bilioni 14 zimetolewa na Benki ya Dunia chini ya Mpango wa kuzijengea uwezo serikali za mitaa(ULGSP), mpango huo unakusudia kuendeleza miundombinu ya Halmashauri za miji na Manispaa 18 za Tanzania Bara ikiwemo Manispaa ya Songea.
Mradi huo ambao ulianza Juni Mosi 2015 ulitarajiwa kukamilika Juni 30,2017.Barabara za Manispaa ya Songea ambazo zipo kwenye mradi huu ni FFU hadi Matogoro yenye urefu wa kilometa 3.2,barabara ya Songea Girl’s hadi Mateka yenye urefu wa kilometa 1.5 na barabara ya Mwembechai hadi Bombambili yenye urefu wa kilometa 2.6.
Barabara nyingine ni Mitumbani hadi Yapenda yenye urefu wa kilometa moja,barabara ya Polisi hadi Stendi ya Mlilayoyo yenye urefu wa kilometa 0.45.
Imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Agosti 13,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa