WAKALA wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula(NFRA) Kanda ya Songea imependekeza kununua mahindi ya akiba ya serikali tani 7000 katika kipindi cha kuanzia Julai 2018 hadi Juni 30,2019.
Mkoa wa Ruvuma katika kipindi cha mwaka 2017/2018 umezalisha mahindi tani 933,284.Akitoa taarifa ya NFRA kwa niaba ya Meneja wa Kanda ya Songea Eva Kwavava katika kikao kilichoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma ambaye aliwakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbinga,amesema mgawo wa tani hizo unazingatia taarifa za uzalishaji wa kila Halmashauri.
Kikao hicho ambacho kimefanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea kimewashirikisha,wabunge wa mkoa wa Ruvuma, wakurugenzi,wenyeviti wa Halmashauri, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea,wakuu wa wilaya, makatibu tawala wa wilaya na watalaam wa kilimo na ushirika.
Viongozi hao kwa pamoja wameridhia mapendekezo hayo na kushauri kutafuta fedha ya kuongeza ununuzi wa mazao kwa sababu tani zilizopendekezwa kununuliwa na serikali ni kidogo ukilinganisha na uzalishaji.
Hata hivyo Kaimu Meneja huyo wa NFRA amesema bei elekezi ya ununuzi wa mahindi na tarehe ya kuanza kununua itatajwa wakati wowote kuanzia sasa baada ya mchakato kukamilika.
Mapendekezo ya malengo ya ununuzi kwa mwaka 2018/2019 katika mkoa wa Ruvuma yanaonesha kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Songea mgawo ni tani 417 wakati kiasi kilichozalishwa ni tani 58,144,Halmashauri ya Wilaya ya Songea tani 1,983.531,kiasi kilichozalishwa ni tani 227,320 na Halmashauri ya Madaba tani 1,216.466 na kiasi cha tani zilizozalishwa ni 148,408.
Kulingana na mapendekezo hayo Halmashauri ya wilaya ya Mbinga imepangiwa kununua tani 1,189.175,kiasi kilichozalishwa ni tani 165,484,Halmashauri ya Mbinga Mji tani 461.976 na kiasi cha tani zilizozalishwa ni 64,288.
Katika Wilaya ya Namtumbo zitanunuliwa tani 1,068.017,kiasi kilichozalishwa ni tani 134,708,Nyasa tani 663.011 na kiasi kilichozalishwa ni tani 64,432 na wilaya ya Tunduru imezalisha tani 70,500 za mahindi na hakuna wa ununuzi.
Katika msimu wa mwaka 2017/2018 Kanda ya Songea ilipangiwa kununua mahindi tani 6,182,hata hivyo kanda hiyo ilinunua jumla ya tani 11,557,529 baada ya malengo kuongezwa mara mbili.
Kaimu Meneja wa NFRA Kanda ya Songea amesema katika kituo hicho kilichopo Ruhuwiko mjini Songea,kuna tani 21,892.924 za mahindi ambayo yanatokana na ununuzi wa misimu miwili ya 2016/2017 na 2017/2018 na kwamba akiba hiyo ipo katika hali nzuri.
Pamoja na kupitisha mapendekezo hayo wajumbe wa kikao hicho wameshauri kipaumbele cha ununuzi kiwe kwa wakulima wadogo badala ya wakulima wafanyabiashara na njia za ununuzi ziwe katika vyama vya ushirika na ununuzi kupitia vituo vya ununuzi vitakavyopangwa katika kila Halmashauri.
Wajumbe hao pia wameshauri mipaka ya nchi isifungwe ili kuruhusu soko la mahindi nje ya nchi,kusimamia ubora za mahindi,kutoa elimu na kuhamasisha wananchi wajitokeze kwenye vituo vya kununulia mazao mara vitakapotangazwa.
Imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Julai 19,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa