KASI ya maambukizo mapya ya virusi vya UKIMWI katika Kata ya Ruhuwiko Manipaa ya Songea mkoani Ruvuma inatishia ustawi wa jamii baada ya kata hiyo kuwa miongoni mwa Kata 10 zenye maambukizi ya kutisha kati ya kata 21 zilizopo Manispaa ya Songea.
Taarifa ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI iliyotolewa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Mtaa wa Ruhuwiko Kanisani,inaonesha kuwa hali ni mbaya ambapo hivi sasa hadi watoto wadogo wapo katika hatari ya kupata maambukizi.
Mwenyekiti wa serikali ya Mtaa wa Ruhuwiko Kanisani Kata ya Ruhuwiko Angelina Haule anaelezea namna watoto wa awali walivyo katika hatari ya kupata maambukizi ambapo ameshuhudia katika Mtaa wa Ruhuwiko Kanisani Baadhi ya watu wametumia mpira ya kujikinga na virusi vya UKIMWI yaani kondom na kuitupa hovyo ikiwa na uchafu ambapo watoto wadogo wameonekana baadhi ya maeneo wakipuliza mipira hiyo hali ambayo inahatarisha afya za watoto hao wasiokuwa na hatia.
"Mimi mwenyewe nimewakuta watoto wanaosoma darasa la awali wakipuliza kondom ambazo zimetumika kwa kweli inasikitisha sana ndugu zangu'',anasisitiza Haule wakati anazungumza na wananchi wake.
Mratibu Kinga(CHAC) katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea Zale Makaburi anazitaja Kata ambazo maambukizi ya virusi vya UKIMWI yapo juu kuwa ni Mateka, Bombambili, Mshangano, Lizabon,Lilambo na Ruhuwiko.
Takwimu zinaonesha kuwa watu 10,097 katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea wanaugua UKIMWI na wapo kwenye dawa hadi sasa ambapo Zaidi ya watu 21,000 katika Manispaa hiyo wanaishi na virusi vya UKIMWI.
Taarifa ya kamati Shirikishi ya kudhibiti UKIMWI iliyotolewa kwenye mkutano wa mwaka wa Baraza la Madiwani uliofanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea,inaonesha kuwa kiwango cha maambukizi katika Manispaa hiyo kimepungua toka asilimia 4.2 hadi kufikia asilimia 3.7.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo Halmashauri ya Manispaa ya Songea ina jumla ya vituo 24 vinavyotoa huduma za Tiba na matunzo kwa waathirika wa ugonjwa wa UKIMWI.
Mratibu wa UKIMWI na tiba katika Manispaa ya Songea Dk.Felista Kibena ameyataja makundi ambayo yanaongoza kwa maambukizi mapya ya UKIMWI kuwa ni watu wanaofanya biashara ya ngono,wanaofanya ngono ya jinsia moja,wanaojidunga sindano na pamoja na wabwia unga na dawa za kulevya.
Kibena amesema idara yake imeamua kutoa elimu ya ukweli kuhusu UKIMWI katika makundi hayo baada ya utafiti kubaini makundi hayo sasa yanaongoza kwa kiwango kikubwa cha maambuzi ambacho ni asilimia 36 sawa na kila watu 100,watu 36 wana virusi vya UKIMWI.
Hata hivyo amesema kiwango cha maambukizo cha watu wa kawaida ni asilimia tano sawa na kila watu 100,watu watano wana virusi vya UKIMWI.
Mkoa wa Ruvuma unashika nafasi ya tano kitaifa ukiwa na maambukizi ya asilimia saba ambapo mkoa wa Njombe ndiyo unaongoza kitaifa ukiwa na asilimia 14.5,nafasi ya pili inashika na Mkoa wa Iringa,ikifuatiwa na Mkoa wa Mbeya kwa nafasi ya tatu na Mkoa wa Rukwa ukiwa nafasi ya tano.
Taarifa imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari wa Manispaa ya Songea
Mei 10,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa