MKURUGENZI wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma Tina Sekambo amesitisha uchinjaji wa nguruwe katika maeneo yote ya Manispaa hiyo tangu Februari mwaka huu, kufuatia kuibuka kwa homa ya nguruwe ambayo haina kinga wala tiba.
Takwimu ambazo zimetolewa na Afisa Mifugo na Uvuvi wa Manispaa ya Songea,Bilaly Mwegeni zinaonesha kuwa homa ya nguruwe(African Swine Fever) katika kipindi cha kuanzia Januari 31,2018 hadi Machi 14,2018 imeua nguruwe 864.
Hata hivyo amesema takwimu hizo za vifo ni matukio ambayo yameripotiwa katika Idara yake ambapo uchunguzi umebaini kuwa zaidi ya nusu ya nguruwe walipo Songea wamekufa kutokana na ugonjwa huo, hali ambayo inataharisha kuteketeza nguruwe katika Manispaa hiyo.
“Takwimu zinaonesha kuwa Manispaa ya Songea ina nguruwe 4581,tukifanya sensa ya idadi ya nguruwe waliobakia katika Manispaa yetu,naamini watakuwa hawazidi 2000,kwa sababu kuna nguruwe wengi wamekufa na takwimu za vifo hazijaletwa ofisini kwetu’’,anasisitiza Afisa Mifugo Mwegeni.
Mwegeni anazitaja kata ambazo zinaongoza kwa vifo vya nguruwe kuwa ni NdilimaLitembo vifo (334),Lizaboni (138), Msamala(90), Matarawe(66) na Ruhuwiko(34) na kata nyingine vifo vya nguruwe ni sio zaidi ya nguruwe watano.
Kutokana na kuenea kwa Homa ya Nguruwe (African swine fever) katika Manispaa na ili kuzuia usambaaji zaidi wa Homa ya Nguruwe Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea aliagiza watendaji wote wa Mitaa na Kata kuanzia sasa wahakikishe hakuna mtu, kuchinja nguruwe, kusafirisha nguruwe,kuingiza na kutoka katika maeneo ya Manispaa.
Hata hivyo uchunguzi umebaini ugonjwa wa homa ya nguruwe upo katika Halmashauri tatu za Mkoa wa Ruvuma ambazo ni Halmashauri ya Manispaa ya Songea,Halmashauri ya Wilaya ya Songea na Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa.
Kutokana na hali hiyo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma imeitisha mkutano wa wadau wa sekta ndogo ya nguruwe,Machi 26 mwaka huu kukutana kwenye ukumbi wa Maliasili mkoa kwa lengo la kujadili mkakati wa kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo na namna ya kudhibiti ueneaji wake.
Ugonjwa wa homa ya nguruwe hauna kinga.Hata hivyo ugonjwa huo hauna madhara kwa binadamu ambapo kitaalam nguruwe aliyekufa kwa ugonjwa huo anatakiwa kuzikwa katika shimo lililopuliziwa dawa ya kuteketeza virusi lenye urefu wa zaidi ya meta moja.
Taarifa imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Machi 25,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa