UGONJWA wa malaria ndiyo unaongoza kwa kusababisha vifo kuliko magonjwa mengine hapa nchini.
Watalaamu wanasema kuwa kuna njia tatu za kupambana na ugonjwa wa malaria njia ya kwanza ni kuhakikisha kuwa watu wote wanaougua malaria wanapata tiba sahihi ya malaria.
Njia ya pili ni kuhakikisha kuwa watu wasiumwe na mbu wa malaria kwa kutumia vyandarua vyenye dawa.
Njia ya tatu ya kutokomeza malaria ni kuangamiza mazalia ya mbu kwa kupuliza dawa.
Utafiti unaonesha kuwa njia ya tatu ya kuangamiza mazalia ya mbu inaweza kumaliza malaria kwa asilimia 100.
Teresia Nyirenda ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Saint Teresa Orphas Foundation (STOF) ambaye anaishi nchini Marekani anasema mazingira ya Tanzania yamekuwa ni mazalio ya mbu hali inayochangia kueneza ugonjwa wa malaria ambao unamaliza maelfu ya watu kila mwaka.
Nyirenda anaitaja njia ya gharama nafuu ya kupambana na mazalia ya mbu kuwa ni kutumia maua na miti ambayo inatumika nchini Marekani ambayo imechangia kumaliza mbu wa malaria katika nchi hiyo.Ameitaja mimea hiyo kuwa ni majivuno na michaichai.
Ugonjwa malaria bado ni tatizo kubwa hapa nchini kwa kuwa ugonjwa huo ndiyo unaoongoza kwa kusababisha idadi kubwa ya vifo ambapo watanzania kati ya 60,000 hadi 80,000 wanakufa kutokana na ugonjwa huo kila mwaka.
Kwa mujibu wa takwimu hizo kila siku watu 291 wanapoteza maisha kutokana na ugonjwa wa malaria wengi wao ni watoto chini ya miaka mitano.
Inakadiriwa kuwa zaidi ya asilimia 93 ya watanzania wanaokadiriwa kufikia milioni 55 wapo katika hatari ya kuambukizwa malaria na hivyo kuifanya Tanzania kuwa nchi ya tatu duniani kuwa na idadi kubwa ya watu wengi walio katika hali hatarishi ya kuambukizwa malaria.
Takwimu kutoka shirika la afya ulimwenguni zinaonesha kuwa kila mwaka watu kati ya milioni 300 hadi 500 duniani wanapata ugonjwa wa malaria, kati yao watu milioni moja na nusu wanakufa kutokana na ugonjwa huo.
albano.midelo@gmail.com,simu 0784765917
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa